HabariLifestyleMombasaNews

WAPWANI WAUNGA MKONO MGOMO WA MADAKTARI

Asilimia kubwa ya Wapwani waunga mkono mgomo wa madaktari unaoendelea kote nchini licha ya kupitia changamoto katika harakati ya kusaka huduma za matibabu kwenye hospitali na zahanati za umma.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la kutetea haki za kibinadamu la HURIA kutathmini athari ya mgomo wa madaktari kwa wakaazi wa kaunti sita za pwani asilimia 73.8 wamebaini kuunga mkono suala hilo wakiamini wana haki ya kupigania haki zao.

Katika kikao maalum na vyombo vya habari mapema leo Mkurugenzi wa shirika hilo Yusuf Lule ameeleza kuwa tathmini hiyo imebaini kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaendelea kusaka matibabu katika  hospitali za umma licha ya wao kuwa na ufahamu kuhusu mgomo huo.

Vilevile amesikitishwa na baadhi ya wahudumu wa katika vituo vya afya wanaopandisha  bei ya huduma za matibabu jambo analolitaja kuwa miongoni mwa vikwazo kwa wananchi kupata huduma bora za afya.

“Wengi wa waliohojiwa katika utafiti huu wanaunga mkono wahudumu wa afya  kugoma  licha ya changamoto zinazowakabili ,asilimia 74 ya walihojiwa wameonyesha kutoridhishwa na jinsi serikali imekuwa ikishughulikia malalamiko ya madaktari kwa kwa miaka mingi.”alieleza Lule.

Kadhalika tathmini hiyo imefichua kuwa asilimia 2 ya wapwani wamegeukia tiba za kiasili na maombi kama mbinu mbadala za kujisaidia  kufuatia mgomo huu kutokana na kutokuwa na fedha za kupeleka wapendwa wao katika hospitali na zahanati za kibinafsi kupata matibabu ikizingatiwa kuwa hali ya uchumi nchini imezidi kuwakeketa wengi.

Shirika hilo limeongeza kuwa huenda athari ya mgomo huu ukawa mbaya zaidi iwapo wahudumu wengine wa afya watachukua mkondo sawia hatua ambayo huenda ikahatarisha zaidi maisha ya wakenya.

Aidha wametoa wito kwa serikali kuchukulia suala hilo kwa dharua na kufanya mazungumzo na madaktari ili kuafikiana kuhusu suluhu ya kudumu kwa manufaa ya wananchi badala ya kutishia madaktari kuwaondoa kazini wakisisitiza kuwa ni nguzo muhimu katika kulinda jamii.

“Wananchi walioshiriki katika utafiti huu walitaka serikali kuheshimu madai ya madaktari,kuweka kipaumbele cha rasilimali ya sekta kwa afya ya umma na kuchukua hatua kwa ahadi walizopewa madaktari kwa miaka mingi.”

Lule vilevile amekemea utepetevu unaoendelezwa na baadhi ya serikali za kaunti katika utekelezwaji wa jukumu la afya kwa nchi ambalo limegatuliwa kwa kuendeleza ufisadi kwenye sekta hiyo na kupelekea kudorora kwa huduma hizo katika hospitali za umma.

BY BEBI SHEMAWIA