HabariNews

‘Mniite Zakayo mniite nini, Tulipe Ushuru Tujenge Kenya,’ Rais Ruto asisitiza

Rais William Ruto ameendelea kutetea Serikali yake dhidi ya ushuru zaidi unaoendelea kutozwa wananchi hapa nchini.

Akizungumza na Wakenya wanaoishi Nchini Marekani katika kituo cha Cob Galeria Atlanta Nchini, Rais Ruto amesema kwamba ushuru huo utasaidia pakubwa kuimarisha Kenya kiuchumi.

“Nyinyi mlioko huku mna risiti za mishahara na risiti za mishahara yenu ina mlolongo ya ushuru ama, n ani fupi ama mrefu? Si mlolongo ya ushuru si ndefu hapa, hivyo ndivyo unavyojenga nchi wenzangu, hujengi nchi kwa sababu ya madeni, ati kukopa hapa au pale, unajenga nchi kutumia ushuru wako mwenyewe, so hata mniite Zakayo mniite nini, lakini tulipe ushuru tujenge Kenya.” Alisema.

Wakati uo huo Rais amesema kwamba mikakati kabambe imewekwa ili kuzuia ubadhirifu wa pesa za umma akiahidi kusaidia kuhakikisha Kenya inapiga hatua kubwa kiuchumi.

“Hakikisho nimewapa Wakenya ni kuwa pesa zao, lazima ziwe salama, fedha zao zitumike vile zilivyopangwa na inavyostahiki na ndio sababu hiyo wiki mbili zilizopita niliidhinisha sheria ya utendakazi wa umma.”

Rais aidha ametoa wito kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini Kenya.

Baadaye, Rais alikutana na Wanadiaspora wa Kenya ambapo alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Wakenya nje ya nchi.

Alieleza kuwa Serikali imeimarisha usajili wa diaspora na uchoraji wa ramani kwa ujuzi na utaalamu.

 

“Tunatengeneza Mkakati wa Soko la Ajira Duniani ambao unalenga uwekaji salama na wenye utaratibu wa Wakenya katika nafasi za ajira nje ya nchi,” alisema.

Alidai kuwa Serikali inaharakisha Mikataba ya Wafanyikazi baina ya Nchi Mbili ili kuwafichua Wakenya kwa fursa mbalimbali na pana.

BY MJOMBA RASHID