HabariNews

CIPK yazindua kampeni ya kuhubiri amani na athari ya mihadarati kwa vijana ukanda wa Pwani

Kampeini ya kuhamasisha vijana eneo la Pwani kuendeleza amani na kujihusisha na miradi ya kujiendeleza imeanza rasmi kaunti ya Mombasa.

Kampeini hiyo inayoongozwa na Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini, CIPK ilizinduliwa wiki jana inawahusisha viongozi wa kidini watakaohubiri amani ikiwalenga vijana kote Pwani kuwahimiza vijana kukumbatia amani.

Katibu Mratibu wa CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa alisema viongozi wanatumia fursa ya kuwepo kwa utulivu nchini kuwahamaisha vijana dhidi ya kutumiwa kuzua vurugu na kutatiza usalama hasa pale wanapotumia mihadarati.

“Hakuna kitu kibaya zaidi kama madawa ya kulevya na ndio maana tumekuwa tunapigana sana kuharamisha ili serikali ikatazae kabisa miraa na mugukaa.

Kwa sababu wanapotumia madawa ya kulevya ni rahisi kwao wao kutumiwa na magenge ya wahuni, magenge ya wahuni wanasiasa na kadhalika,” alieleza sheikh Khalifa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu katika baraza hilo, Balozi Sheikh Mohammed Dor alieleza kwamba kampeini hiyo iliyoanza rasmi hapa Mombasa kwa kuwakusanya mamia ya vijana itaendelezwa kote Pwani ikilenga kuwahamaisha vijana kuhusu umuhimu wa kuzingatia elimu na kutumia mitandao ya kijamii katika njia inyofaa.

“Tutaendelea kaunti mbalimbali na khususan ni masuala ya vipi kumlea yule kijana ambaye ashaanza kufikia kuanzia miaka 15  kwenda juu umuhimu mwanzo apate ilmu.

Na twawambia wazazi ya kwamba hakuna urathi mzuri kama urathi wa ilmu.

Ukiangalia mas’ala ya social media, ukiangalia magroup ambayo wao wanaungana nayo mara kwa mara ambapo wazazi wako mbalimba na wao,warsha kama hizi ndio zitawafanya vijana kwenye ndhia ya kuwakumbusha,” alisisitiza sheikh Dor.

Kampeni hiyo ilianza huku visa vya utovu wa usalama, utumizi wa mihadarati vikiripotiwa kuongezeka kila uchao kaunt ya Mombasa na maeneo mengine ya ukanda wa pwani hata taifa kwa jumla.

Moja ya hatua iliyokosolewa nchini ni vijana kutumiwa kuharibu maandamano ya amani ambayo yalikuwa yanaongozwa na vijana wa kizazi cha GEN-Z kupinga serikali ya rais William Ruto.

BY MAHMOOD MWANDUKA