LifestyleMombasaNews

Wazazi watakiwa kuzidisha uangalifu kwa wanao shule zinapofungwa kwa likizo ndefu.

Wazazi wametakiwa kuwa waangalifu mno kwa wanao hasa msimu huu ambapo wanafunzi wanarudi nyumbani baada ya shule kufungwa kwa likizo ndefu.

Wanafunzi wakiendelea kurudi nyumbani kufuatia kukamilika kwa muhula wa tatu na kupelekea shule kufungwa kwa likizo ndefu wazazi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuepusha wanao kupotokwa kimaadili.

Erick Karisa Mgoja ofisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la KIlifi Social Justice Centre, anasema wazazi kuzidisha uangalifu kwa wanao kutasaidia kuwepo kwa usalama katika jamii na kuepukwa kushuhudiwa kwa visa vya mimba za utotoni hasa wakati huu ambapo wanafunzi wako nyumbani kwa likizo ya takriban miezi miwili.

Amesistiza kuwa licha ya wazazi wengi kupitia hali ngumu za uchumi, jukumu la kuwachunga wanao lazima wahakikishe wanalitekeleza kikamilifu.

“Kwasababu ya gharama ya maisha vile ambavyo imepandawazazi wanakuwa na shughuli nyingi za kutafutia familia na mara nyingi watoto wanawachwa peke yao. Na hapo ndipo mambo mengi yanayosababisha utovu wa usalama hutokea, na matukio mengi ambayo yamesababisha vijana wadogo kujiingiza kwenye makundi ya kihalifu na pia tumeona wasichana wadogo wakipata mimba wakati huu.

“Kwa hivyo letu sisi kama shirika ni kutoa wito kwa wazazi waweze kuwa waangalifu zaidi na kila mmoja aweze kutekeleza jukumu lake ili watoto wetu wazidi kuwa salama.” alisema Mgoja.

Kwa upande wake Kalugho Menza Kalugho wakili wa nyanjani katika shirika la Kilifi Social Justice Centre ameeleza kuwa wazazi wanafaa kutumia mbinu ya kukaa na kuwaongelesha wanao maarufu “positive parenting” ili kufahamu na kutatua changamoto wanazopitia watoto kwenye familia.

Aidha amewasihi wazazi kujizatiti na kuwapongeza ili kuwatia motisha wanapofanya vyema na vile vile kuwatia moyo wanapofeli shuleni huku akiwataka kuwafunza dini wanao ili wawe watoto wema.

“Haya mambo ya “positive parenting” ni jinsi ya vile wazazi wanaweza kukaa na wanao na kuwaongoza kwa kuwaongelesha kuhusu zile tabia ambazo ni za sawa na zile ambazo sio sawa ili waweze kuwa watoto wema na watakao kuwa wazuri katika jamii. Na pia kuwapekeleka katika sehemu za kuabudu wajue maneno ya Mungu.” alisema Kalugho.

Erickson Kadzeha.