Rais William Ruto amekutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) anayeondoka Moussa Faki Mahamat huko Kilgoris kaunti ya Narok.
Wawili hao wamefanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa mageuzi ya AUC yaliyaofikiwa ili kutumika katika kusukumu ajenda za Bara la Afrika.
Katika mtandao wake wa X rais Ruto amesema alikutana na Faki huko nyumbani kwake Kilgoris, Kaunti ya Narok, ambapo pia walijadili mageuzi ya AU na uchaguzi ujao wa Mwenyekiti wa tume ya Afrika, AUC.
Waziri Mkuu wa zamani nchini Raila Odinga amelenga kumrithi Moussa Faki katika nafasi hiyo ya Uenyekiti wa AUC katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Rais Ruto ameunga mkono azma ya Odinga kuwania nafasi ya AUC, na kuwataka Wakenya na washirika wa kimataifa kumuunga mkono kuwania kwake.
Katika uchaguzi huo ulioratibiwa kufanywa Februari mwakani, Odinga atachuana na Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.
Itakumbukwa kuwa akizungumza wakati wa mdahalo wa Mjadala Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, Raila alieleza kuwa Afrika, inayojumuisha mataifa 55, inapaswa kuwa na uwakilishi ndani ya baraza hilo ili kukuza maslahi ya bara hilo wakati wa kujadili usalama wa kimataifa.
By Mjomba Rashid