Waziri wa usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen ameagiza kukamatwa kwa wanasiasa wanaodaiwa kufadhili magenge ya uhalifu.
Akizungumza hapa mjini Mombasa katika kikao na maafisa wa usalama, Waziri Murkomen ameagiza maafisa wa polisi kukabiliana vilivyo na magenge hayo yanayoitatiza usalama eneo la Pwani.
Waziri Murkomen aidha ameonya kuwajibishwa na kufutwa kazi mara moja kwa maafisa wa usalama wanaozembea kazini, huku akiahidi kupandishwa vyeo kwa watakaowajibika.
Waziri huyo ambaye ameanza ziara ya kiusalama eneo la Pwani, amebaini kuwa masuala mengine atakayoshughulikia na wadau mbalimbali katika ziara yake hii ni suala la ulanguzi na utumizi wa mihadarati ambalo limekuwa changamoto na kikwazo cha usalama Pwani.
“ Suala amabalo serikali inapania kuangazia katika ukanda huu wa pwani ni kuhusu kudorora kwa usalama pamoja na utumizi wa dawa za kulevya hasa miongoni mwa vijana ambayo ni kati ya changamoto kubwa zinazowakumba wa pwani.” Alieeleza Murkomen.
Wakati uo huo Murkomen amebaini kuwa machifu watano waliotekwa nyara na wanamgambo wa Alshabab eneo la Elwak kaunti ya Mandera mnamo miezi miwili iliyopita hatimaye wameachiliwa huru, baada ya Kenya kupeleka vikosi vilivyoshirikisha viongozi wa jamii kwenda Somalia kujadili kuachiliwa kwao.
Waziri huyo amesema kuwa machifu hao wako salama mikononi mwa vikosi vya Kenya na wanatarajiwa kuwasili nchini kuungana na familia zao.na kwamba serikali ilipeleka baada ya kukamilisha utaratibu ufaao.
“ Tuna taarifa njema kwamba machifu wetu watano waliotekwa nyara huko Mandera wameachiliwa na wanatarajiwa kuungana na familia zao.
Hii ni kufuatia juhudi za pamoj za serikali kuu na ile ya kaunti ya Mandera pamoja na jaamii ya eneo hilo na hatimaye juhudi zetu zimefua dafu.” Murkomen alifichua.
Machifu hao walitekwa nyara mnamo Februari 2025 siku moja kabla ya ziara ya rais William Ruto eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi na wanaamika kuwa walikuwa wakizuiliwa katika nchi jirani ya Somalia na wanamgambo wa Alshabab.
By Mjomba Rashid