Habari

Magoha agadhabishwa na idadi ndogo ya polisi kulinda mitihani……

Mtihani wa KCPE umeingia siku ya pili hii leo, huku zoezi hilo likiendelea vyema katika maeneo mengi ya taifa.

Leo Jumanne watahiniwa wanafanya somo la Sayansi, kisha Kiswahili Lugha na kumaliza siku kwa somo la Kiswahili Insha.

Waziri wa Elimu George Magoha amekuwa katika kaunti ya Machakos kusimamia shughuli ya usambasaji wa karatasi za mtihani.

Magoha hata hivyo alionyesha kutoridhika kwake na kiwango cha ulinzi katika vituo vya mitihani.

Waziri alihoji kwa nini ni polisi mmoja pekee aliyekuwa ametumwa kushika doria katika vituo vya kufanyia mitihani katika kaunti ya Machakos badala ya polisi wawili kama inavyohitajika.

Mtihani wa KCPE unatarajiwa kukamilika hapo kesho huku kukiwa hakuna visa vyovyote vya udanganyifu vilivyoripotiwa.