Habari

Jaji David MARETE asema hana matatizo ya kiakili kama inayodaiwa……

Mahojiano ya kumtafta jaji mkuu nchini yameingia siku ya nne hii leo, wanne kuhojiwa akiwa ni jaji wa mahakama ya leba David Marete na ambaye pia ni mhadhiri wa sheria katika chuo kikuu cha African Nazarene.

Jaji Marete akijieleza amesema suala la kwanza atakaloshughulikia ni la kesi kurundikana mahakamani na swala la teknolojia kupewa kipau mbele akisema maswala haya mawili yanaendana.

Aidha Marete amesema kuwa wafanyikazi pia ni lazma waongezwe kwenye tume ya huduma za mahakama JSC ili kukuza utendakazi wa mahakama.

Akiendelea kujieleza, Jaji Marete amesema kwamba haogopi kufanya maamuzi yoyote yatakayomuweka katika nafasi ya kutekeleza majukumu yake.

Wakati huo huo Jaji Marete amelazimika kufafanua zaidi kwamba hana matatizo ya akili jinsi cheti chake kinavyothibitisha kwamba ni mtu mwenye ulemavu kilivyosema.

Akijibu maswali ya jaji Mohammed Warsame amesema kumekuwa na matatizo wakati alipokuwa anasajiliwa kukichukua cheti hicho, na kwamba tatizo alilonalo ni la macho akisema pia anaugua kisukari na wala sio akili.

Amesema matatizo ya kiafya aliyonayo hayajamzuia kutekeleza majukumu yake, na wala hayawezi kumzuia kutekeleza wajibu wake iwapo ataidhinishwa kuwa jaji mkuu.