Habari

Wanafunzi 15 Malindi waliopata alama 350 na zaidi wafadhiliwa…..

Takriban wanafunzi 15 waliopata alama 350 na zaidi Wadi ya Kakuyuni, Malindi kaunti ya Kilifi watanufaika na mpango wa serikali ya kaunti hiyo wa kugharamia masomo yao ya shule za upili.

Kulingana na Mwakilishi Wadi wa Kakuyuni Nixon Mramba mpango huo umekuwa ukigharimu zaidi ya shilingi Millioni tatu kuwalipia karo kila mwaka wanafunzi waliofanya vyema zaidi eneo hilo.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupokea wanafunzi watakaoingia kwenye mpango huo Mramba amedokeza kuwa serikali ya kaunti inalenga kupiga vita umaskini miongoni mwa jamii kwa kuweka kipaumbele maswala ya elimu.

Kwa upande wao Cornelius Kahindi Karisa na na Dena Karisa Wyclife, wameelezea matumaini ya kutimiza ndoto zao kupitia ufadhili huo,wakidai hawakuwa na matumaini ya kujiunga na shule za upili kutokana na hali ya uchochole katika familia yao.

Mama ya watoto hao kwa jina Mapenzi Karisa Katana amesema amelazimika kuuza mboga kwa zaidi ya miaka 6 kusomesha watoto hao baada ya baba yao mzazi kuaga dunia.

Bunge la kaunti hiyo hutenga jumla ya shilingi milioni 350 kila mwaka kufadhili elimu ya wanafunzi kaunti hiyo.

By Correspondent Joseph Yeri