HabariNews

Utovu wa usalama Laikipia wadaiwa kusababishwa na viongozi wakuu serikalini…….

Gavana wa Laikipia Nderitu Mureithi na mbunge wa Laikipia kaskazini Sarah Lekorer wameibua madai kwa utovu wa usalama katika eneo la Laikipia magharibi kwamba unachochewa na baadhi ya viongozi wakuu serikalini.

Wakihojiwa na idhaa moja, viongozi hao wamedai kuwa baadhi ya viongozi wakuu serikalini wanamiliki mifugo wanaolishwa kwenye mashamba binafsi yanaokaliwa na wavamizi hao.

Aidha wamedai kwamba wavamizi hao wanafadhiliwa na kupewa bunduki kuwavamia wakaazi huku wakitoa changamoto kwa mshirikishi wa utawala wa bonde la ufa George Natembeya kuwaambia wakenya ukweli kuhusu kinachojiri Laikipia.

Lekorer aidha amepuuza madai kwamba uvamizi huo unasababishwa na mashidano ya maeneo ya kulisha mifugo na rasilimali za eneo.

Mapema hii leo Natembeya alisema majambazi wanaotatiza usalama eneo la Laikipia wamejihami kwa silaha hatari ambazo ni tofauti kabisa na bunduki aina ya AK47 wanazomiliki polisi eneo hilo suala ambalo linawapatia changamoto maafisa wa polisi kuwakabili.

Akihojiwa na runinga ya KBC, Natembeya amesema kwa sasa wanakabiliana na majambazi ambao wamejihami sawa sawa, akisema idadi ya bunduki zinazosambazwa eneo hilo haiwezi kukisiwa huku akisema licha ya hilo majambazi hao hawawezi kuwa wamejihami zaidi ya serikali.

Hata hivyo Natembeya amesema hatua ya serikali kuwapokonya bunduki maafisa wa polisi wa akiba yaani Kenya police reserve ndio imechangia majambazi hao kushadidisha mashambulizi.

Kauli yake inakuja baada ya hali tete kuendelea kushuhudiwa katika eneo hilo la Laikipia magharibi licha ya oparesheni ya kiusalama iliyoanza kutekelezwa kuwakabili wezi wa mifugo na wavamizi.

Saa chache baada ya oparesheni hiyo kuanza na amri ya kutotoka nje kuazia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi kuanza wavamizi hao wameivamia shule ya msingi ya Mirigut na kuitetekeza.

BY NEWS DESK