HabariNews

HUENDA MPANGO WA MAGEUZI WA MAMLAKA YA KEMSA KUGONGA MWAMBA.

Mpango wa mageuzi katika usimamizi wa mamlaka ya usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu Nchini KEMSA huenda ukagonga mwamba baada ya daktari mmoja kuelekea Mahakamani.

Daktari Magari Gikenyi ameiambia Mahakama kwamba anafahamu mpango wa kuweka mamlaka hiyo chini ya usimamizi wa Jeshi na maafisa wa Shirika la Huduma za vijana, jambo ambalo amelitaja kuwa kinyume na sheria.

Katika utetezi wake Gikenyi amekariri kwamba licha ya mpango huo kuwa na malengo mazuri, umefanywa pasi na kuzingati maslahi ya wafanyikazi ambao wiki iliyopita walitakiwa kufanya kazi nyumbani kwa siku 30.

Wakati uo huo Gikenyi amesema kwamba uamuzi huo umeafikiwa kabla ya suala kuu la ufisadi lililochunguzwa na Kamati ya Bunge, kushughulikiwa jinsi ilivyopendekezwa.

Haya yanajiri huku ikiarifiwa kwamba wengi wa wafanyikazi walioagizwa kufanyia kazi nyumbani hawawezi kutekeleza majukumu yao kwa kutoweza kutounganishwa katika mifumo ya kiteknolojia waliotegemea wakiwa ofisini huku hali hiyo ikiathiri hali ya utendakazi.

Wiki iliyopita mwenyekiti wa afya Bungeni Sabina Chege pia alidokeza kuhusu mpango wa kuialika Bodi ya KEMSA ikiongozwa na Mary Mwadime kufikia mbele yake na kujieleza kuhusu hatua zilizochukuliwa.

Ni hali inayoshuhudiwa wakati ambapo mjadala mkali unaendelea kuhusu usimamizi wa KEMSA na viongozi mbali mbali wakilizungumzia suala hilo katika majukwaa mbalimbali wikendi, miongoni mwa waliozungumza ni pamoja na  mbunge wa Mwingi Magharibi Charles Nguna ,mwakilishi wa KIKE wa kaunti ya Machakos Joyce Kamene, mbunge wa Bobasi  Innocent Obiri pamoja na mbunge wa Kiminini Daktari Chris Wamalwa.

BY NEWS DESK