HabariNews

Viongozi na Idara za Usalama Kwale watakiwa Kuimarisha vita Dhidi ya Mihadarati

Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini Salim Mvurya amewataka viongozi wa Serikali Kuu pamoja na Idara ya Usalama katika kaunti ya Kwale kutolegeza Kamba katika vita dhidi ya mihadarati.

Akizungumza huko Makwenyeni wadi ya Vanga eneo bunge la Lungalunga, Waziri huyo aliwahimiza viongozi hao pamoja na idara ya usalama kutekeleza operesheni ya kudhibiti dawa za Kulevya kama ilivyopitishwa na Baraza la mawaziri.

Mvurya amelitaja tatizo la mihadarati kama chanzo kikubwa cha kurudisha nyuma maendeleo ya kaunti hiyo hasa kwa Vijana wengi waliotumbukia katika janga Hilo.

Wakati uo huo  Mvurya anawataka wakaazi wa kaunti hiyo kushirikiana na maafisa wa Usalama na kufichua walanguzi wa dawa za Kulevya.

Huku hayo yakijiri, Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza ameitaka idara inayosimamia kudhibiti matumizi ya mihadarati NACADA kuorodhesha Mugokaa miongoni mwa dawa za kulevya kwa kuwa umeleta athari zaidi kwenye jamii.

Akizungumza mjini Kwale Tandaza amesema ipo haja ya serikali kuu kupiga marufuku utumizi wa Mugokaa na pia wanaouza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema ni kutokana na madhara kushuhudiwa kwa vijana wengi hasa waraibu kudhoofika kiafya na kukosa mwelekeo.

BY BINTIKHAMIS MOHAMMED