HabariNews

Seneta Miraj alilia madaktari wanaogoma kurejea kazini mazungumzo Yakiendelea

Gumzo linaendelea kutawala kuhusiana na mgomo wa madaktari unaoendelea na hatua ya serikali kusisitiza kuwa haina fedha kutekeleza matakwa yao.

Seneta maalum kaunti ya Mombasa Miraj Abdillah ni kiongozi wa hivi punde kujitokeza kuzungumzia kuhusu mzozo ulioibuka, akisema kuwa baadhi ya matakwa ya madaktari kamwe hayawezi kutekelezeka.

“…Rais wetu William Ruto hana kuumauma maneno, hajui kudanganya, amesema kile ambacho kiko katika hiyo CBA hakitawezekana kufanyika katika wakati huu…” alisema.

Seneta huyo mteule wa chama cha UDA amedai kuwa mapendekezo yaliyoko kwenye mkataba wa makubaliano ya mwaka 2017 yalitumika kisiasa kuwashawishi madaktari kusitisha mgomo wao wakati huo wa uongozi wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Akizungumza huko Naivasha Miraji alisema kuwa kukubaliwa kwa makubaliano hayo ya mwaka huo hakukuzingatia uwezo wa kifedha wa taifa na hata serikali ya wakati huo ilishindwa kutekeleza mkataba huo.

Tumeipata Serikali ikiwa kwenye wakati mgumu sana, hasa haya mambo mengine yalifanyika huko nyuma,” alisema.

Miraj hata hivyo aliwasihi madaktari kurejea kazini huku mazungumzo ya kutafuta mwafaka yakiendelea akiwataka viongozi kuacha kumshtumu Waziri wa afya Susan Nakhumicha.

Wananchi wanaumia watoto wanapata shida, mimi nawanyenyekea madaktari wetu mrejee kazini tukizungumza vile tutatatua haya, tuzungumzie yale yataleta natija na suluhu ya kudumu tuache kuingilia Waziri, tuache kumuingilia kwa sababu ni mtoto wa kie.” Alisema Miraj.

Haya yanajiri huku mgomo wa madaktari ukiingia siku ya 30, tangu kuanza kwake mnamo Machi 14, 2024, huku madaktari chini ya muungano wao KMPDU wakishikilia kutorejea kazibi Serikali itakapotekeleza matakwa yao jinsi yalivyoafikiwa katika Mkataba wa Makubaliano (CBA) 2017.

BY MJOMBA RASHID