HabariNews

SENETA WA NANDI AWASILISHA MSWADA BUNGENI KUONGEZA MUHULA WA RAIS HADI MIAKA SABA

Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei amewasilisha mswada katika Bunge la Seneti akipendekeza katiba ifanyiwe marekebisho ili muhula wa uongozi wa Rais na viongozi wengine uwe wa miaka saba badala ya mitano jinsi ilivyo kwa sasa.

Katika mswada huo ulioko mbele ya kamati ya Haki na Masuala ya sheria katika Bunge la Seneti, Seneta Cherargei anapendekeza katiba kufanyiwa marekebisho ili kurefusha hatamu ya uongozi wakiwemo rais, magavana na wabunge.

Katika mswada wake aliouwasilisha bungeni Seneta huyo wa Nandi anapendekeza marekebisho kufanywa katika kifungu cha 101, 177 na kile cha 180 cha ibara ya katiba ili kufanikisha masuala kadhaa yakiwemo kuongeza hatamu ya uongozi wa rais, wabunge, magavana na wakilishi wadi kutoka muda wa miaka mitano ilivyo kwa sasa hadi miaka saba.

Kadhalika seneta huyo wa Nandi mbali na kutaka Ofisi ya Waziri Mkuu kubuniwa, pia anapendekeza Bunge la Seneti lipewe mamlaka ya kuwapiga msasa mawaziri, Mwanasheria Mkuu, Mkaguzi wa Bajeti, Inspekta Jenerali wa polisi, Jaji Mkuu na majaji wengine kabla ya kuingia ofisini.

Mwandani huyo wa karibu wa Rais William Ruto analitaka bunge la kitaifa lisalie na jukumu la kuwapiga msasa mabalozi huku jukumu la kuidhinisha kupelekwa kwa maafisa wa vikosi vya ulinzi katika shughuli za kudumisha amani liafikiwe na kuidhinishwa na mabunge yote mawili.

Iwapo mswada wa Seneta Cherergai utapitishwa, huenda serikali za kaunti zikafaidi pakubwa, kwani seneta huyo katika mswada wake anapendekeza mgao wa asilimia 40 kwa Serikali za kaunti kama njia mojawapo ya kuboresha ugatuzi.

Kuhusiana na michakato ya kuwabandua mamlakani magavana au manaibu wao, mswada huo unapendekeza mahakama ya upeo kusikiliza na kutoa uamuzi dhidi yao huku pia mahakama zikitakiwa kufanya uamuzi wa kesi katika kipindi cha siku thelathini.

Iwapo pendekezo hilo litapitishwa na kamati ya sheria inayoongozwa na seneta wa Bomet Hillary Sigei na kuidhinishwa na spika Amason Jeffa Kingi, mswada huo utachapishwa na kuwasilishwa rasmi katika bunge la seneti kwa usomaji wa kwanza.

BY ISAIAH MUTHENGI