HabariNewsSiasa

Wafula Chebukati Apoteza Nafasi ya Kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini, IEBC, Wafula Chebukati amepoteza nafasi ya kuwa jaji wa mahakama ya Rufaa.

Hii ni baada ya jina lake kukosa kujumuishwa miongoni mwa watakaohojiwa kuchukuwa wadhfa huo na Tume ya Huduma za Mahakama, JSC.

Chebukati alikuwa miongoni mwa Wakenya 82 waliokuwa wametuma maombi kujaza nafasi 11 za majaji wa mahakama ya rufaa.

Hata hivyo Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imeorodhesha majina ya Wakenya 41 waliofuzu na kuafikia vigezo vya kupita hatua ya kwanza ya mchujo.

Wakati uo huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mpito ya Uchaguzi (IIEC) Ahmed Is-hak Hassan ameorodheshwa kuwania kujaza nafasi hizo kumi na moja.

Wengine waliorodheshwa ni majaji wa mahakama kuu Chacha Mwita, Grace Nzioka, Alfred Mabeya, James Wakiaga, Jeras Ngaya na Hedwig Ongudi miongoni mwa wengine.

Mahojiano ya kujaza wadhfa huo yamepangwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu.

BY MJOMBA RASHID