HabariNews

Wafanyabiashara Wadogo Kunufaika Na Ujenzi Wa soko Jipya Kilifi

Biashara zinatarajiwa kuimarika mjini Kilifi kufuatia mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo wadogo kuzinduliwa rasmi. Soko hilo linalojengwa kwa awamu litakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya wafanyabiashara 150 ambao kwa sasa wanafanya biashara zao kando ya barabara mjini humo baada ya vibanda vyao kubomolewa tangu mwezi Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa diwani wa Sokoni eneo bunge la Kilifi kaskazini Ray Katana Mwaro, ujenzi wa soko hilo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 12, na kuchukua muda wa miezi 6 kukamilika unalenga kuweka mazingira bora ya kuendeleza biashara.

Mwaro amesema katika awamu ya kwanza kutajengwa vibanda 54 huku nje ya soko hilo kukiwekwa makasha yaani “containers” ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanapata nafasi.

“Hivi leo tumekuwa na shughuli ya kupeana sehemu ya ujenzi wa mradi wa soko ambapo kutajengwa vibanda 54 katika maeneo ya Survey na lengo lenyewe ni kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Pia kuna vibanda 120 zilitengezwa kwenye makasha karibu na benki ya Equity mwanakandarasi anaendelea na kazi na mradi wenyewe utagharimu takriban shilingi milioni 12 ambayo kwa miezi sita itakuwa iko tayari.” alisema Mwaro.

Kwa upande wake ofisa wa msimamizi wa majengo kaunti ya Kilifi Ruwa Nzai amesema gharama ya jengo hilo lenye urefu wa futi zaidi ya 100 na upana wa zaidi ya futi 60 inaonesha ubora utakao kuwa kwenye ujenzi wake.

“Jengo lenyewe liko na urefu wa futi 102 na upana wa futi 60 huo ndio ukubwa kwa upande wa hilo jengo. Lakini kwa upande wa gharama sababu kuna vile ofisi ya wahandisi inataka vile jengo liwe hatuliangalii liwe la miezi miwili kasha liwe limeanguka tunataka lidumu kwa muda mwingi kama miaka 50 ndio maana liko na gharama.” alisema Nzai

Benjamin Musembi muwakilishi wa wafanyabiashara wadogo wadogo katika barabara ya Absa hadi Rubis mjini Kilifi ameeleza kuwa soko hilo litawasaidia kujiimarisha tena kiuchumi baada ya wengi kufilisika kutokana na kuvunjwa kwa vibanda vyao.

“Kwa hivyo huu mradi utatusaidia kama wafanya biashara kwasababu zile changamoto tulizopitia katika hii barabara ni nyingi hasa tuliokuja vunjiwa na ikawa ni shida kukimbizana na askari wa kaunti hawataki tupange vitu vyetu. Lakini baadae tukaruhusiwa tupange vitu vyetu chini hawakutaka tujenge mahema na unajua vile jua lilivyokuwa kali, mali zetu zikaharibika, zikaungua baadae msimu wa mvua ukaanza hapo sasa ndio tukapata hasara nyingi kwasababu wamekataa tujenge mahema wanataka tupange vitu chini na kuna nyesha hiyo kwetu imekuwa changamoto sana. Wafanyabiashara wengi wamefilisika sabau wengi mapato yao yalikuwa hapa na hasa wale walio na mikopo.” alisema Musembi.

ERICKSON KADZEHA