HabariNewsSiasa

Waziri wa Kilimo Aepuka Shoka la Kumtimua Uongozini

Hatimaye waziri wa Kilimo Mithika Linturi ameponea shoka la kubanduliwa mamlakani.

Kamati ya bunge ya wanachama 11 ya Bunge la kitaifa iliyotwikwa jukumu la kumchunguza na kusikiza hoja za pande husika imesema madai dhidi ya waziri huyo hayakuwa na msingi.

Akitoa ripoti yake bungeni mnamo Jumatatu Mei 13, Mmwenyekiti wa kamati hiyo Naomi Waqo amemwondolea mashaka dhidi ya madai kuhusu kukiuka sheria na katiba katika utendakazi wake na kutekeleza uhalifu kuhusiana na Sakata ya mbolea ghushi.

Bw. Spika Kufuatia madai yaliyoibuliwa katika hoja iliyowasilishwa hapa Bungeni, Kamati hii imekuja na ripoti kwamba madai hayo yote hayana uzito… alisema Bi. Waqo Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Hata hivyo hatua hiyo imezua mjadala bungeni huku wabunge wanaoegemea mrengo wa upinzani wakishikilia kuwa Waziri Linturi ameonyesha utepetevu na hana uwezo wa kuongoza wizara hivyo basi alipaswa kuondolewa uongozini.

“Hili Bunge haliwezi kutekwa nyara na kutumiwa kiholela tu, kuona hoja hii; suala hili la mbolea linavyoenda namna hii ni hatari kupuuzwa na sasa tumeruhusu kuingia dawa ghushi, maji ghushi na watakaoathirika zaidi ni Wakenya wa chini.” Alisema Junet Mohammed, Mbunge wa Suna Mashariki.

Opiyo Wandayi Kinara wa Wachache Bungeni ameongoza wabunge wa upinzani akidai kuendelea kupuuzwa kwa kilio cha wakulima wa Kenya walioathirika na Sakata hiyo ya mbolea ghushi, na kwamba katika taifa lenye misingi ya demokrasia waziri Linturi alipaswa kujiuzulu kutokana na uamuzi wa awali wa wabunge.

Kufuatia kura ya wabunge wengi Alhamisi iliyopita wabunge 149 waliunga mkono dhidi ya 36 waliopinga, sidhani suala hili lingefika hadi hatua ya kamati. Katika yenye demokrasia halisi punde tu bunge hili lilipopiga kura kwa wingi kumtimua Linturi, angekuwa waziri huyu ashajiuzulu na kushindwa kujiuzulu Mamlaka ilipaswa imfute kazi…” alisema Wandayi.

Otiende Omollo, Mbunge wa Rarieda: Bwana Spika Sisi kama bunge tuliashiria wazi Waziri anapaswa kujiuzulu lakini kamati hii imeshindwa kuheshimu bunge hili kwa jumla, katika demokrasia halisi na ya uhakika kura dhidi ya waziri huyu ingemfanya Waziri huyu ajiuzulu kabla kufikia suala la kamati kufanya kazi yake lakini sasa hakuna demokrasia katika utawala huu. Sasa basi kitakachowaokoa wakulima wa Kenya ni hatua ya Rais mwenyewe anaweza kuchukua kuwaokoa Wakenya.”

Hata hivyo wabunge wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wameisifia ripoti hiyo wakisema kwamba hoja ya kumbandua Waziri Linturi haikuwa na mshiko wala msingi wowote na kwamba kamati ilifanya kazi yake pasi msukumo wala kuingiliwa kati.

“Mwenyekiti wa Kamati hii ni Kasisi n ani mtu wa maadili ya hali ya juu, hajakuwa na malengo fiche bwana Spika…” alisema Mbunge Sylvanus Osoro.

Kimani Ichungw’ah ni Kiongozi wa wengi katika bunge la Kitaifa na alikariri kuwa wabunge hawapaswi kuongozwa na hisia zao wakati wa kuwasilisha mswada au hoja ya kumbandua Afisa yeyote uongozini.

Kumbandua Waziri si suala la kupiga kura na kufanya uamuzi unaoendeshwa na hisia, si suala la kuamua iwapo unampenda mtu au humpendi…ni funzo kwa wengine sasa ni lazima tuhakikishe muda wotote ukitaka kumbandua Waziri au afisa yeyote wa serikali sharti izingatie kile kilicho kwenye sheria.” alisema Ichung’wah.

Haya yanajiri kufuatia kamati ya bunge ya wanachama 11 kumwondolea mashaka ya kuhusika na sakata ya mbolea ghushi Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, ambapo 7 kati ya wanachama hao walipiga kura ya kutombandua, 4 wakipiga kura kuunga mkono kubanduliwa kwake.

BY MJOMBA RASHID