HabariNews

Gavana Mwangaza gizani hoja ya tatu ya kumbandua afisini ikiwasilishwa tena bungeni

Hatima ya Gavana wa Kaunti ya Meru Kawira Mwangaza Kwa Mara nyingine inasalia mashakani baada ya hoja nyingine ya kumbandua mamlakani gavana huyo kufikishwa katika Bunge la Kaunti hiyo.

Notisi ya mswada wa kumbandua Mwangaza ofisini imewasilishwa na mwakilishi wadi Zipporah Kinya Katika Bunge la Kaunti ya Meru kwenye Kikao cha adhuhuri  mnamo Julai 17, 2024 cha Bunge Hilo.

Gavana Kawira Mwangaza anakabiliwa na shutuma mbili  mojawapo ikiwa ni matumizi mabaya ya ofisi na mamlaka yake na pia madai ya matumizi mabaya rasilimali za kaunti ya Meru.

Kuwasilishwa Kwa Mswada huo kumefikisha idadi ya miswada dhidi yake kuwa mitatu kuwahi kufikishwa mbele ya spika wa Bunge la Kaunti hiyo Ayub Bundi ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu Mwangaza aingie mamlakani.

Itakumbukwa kuwa jaribio na michakato ya awali ya madiwani wa Bunge hilo ya kutaka kumtimua Mwangaza iliogonga mwamba mwaka Jana na Juzi baada ya gavana huyo kunusuriwa na Bunge la seneti.

Je, Mwangaza wa Mwangaza utamnusuru Kwa Mara nyingine au hatima yake itazimwa mswada huo ukifaulu?

BY NEWS DESK