HabariNews

Viongozi wa dini wahimiza kutoondolewa kwa Bima ya afya nchini NHIF

Serikali imetakiwa kutathmini upya hatua ya kuhamisha huduma za afya kutoka kwa bima ya kitaifa ya afya nchini NHIF hadi kwa hazina ya afya ya Jamii SHIF.

Katibu mkuu wa baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu nchini CIPK Balozi Sheikh Mohamed Dor alisema hatua hiyo itakuwa na athari kubwa kwani itamlazimu mwananchi wa kawaida kugharamika zaidi.

Mfumo huo ambao mapema mwezi Julai, 2024 Mahakama Kuu iliutaja kama unaokiuka katiba, Kiongozi huyo wa kidini alionya kwamba huenda ukatumika kama chombo cha taasis binafsi zitakazotwikwa majukumu ya kuendesha bima hiyo kujilimbikizia faida kubwa.

“Tubakie kwenye NHIF sio kwenda SHIF, Kwa sababu SHIF tushasikia ya kwamba watapewa kampuni private wamanage.

Hizo kampuni ni trading organisations watatia faida kwenye kila transaction watakayofanya, sisi wakenya ndio tutakaoumia Muheshimiwa rais.” Alisema sheikh Dor. 

Kuhusu matozo ya ushuru katika mswada wa fedha 2024 uliozua ghadhabu ya maandamano, Sheikh Dor aliishauri serikali kila mwaka inapoandaa mswada wa fedha, kutozingatie nyongeza za ushuru pekee.

Aliitaka serikali kubuni mbinu maalum za kupunguza ushuru ili kumpunguzia gharama mwananchi wa kawaida.

“Ikiwa ni lazima mas’ala ya yakueka kodi iwekwe yenyewe wasema friendly taxation.

Ni lazima kweli kwamba kila mwaka kuwe na finance bill, ni lazima ulimwengu mzima, lakini si lazima kuongeza kodi kila mwaka. Kuna nchi ngapi ambazo kwenye finance bill za mwaka ule wanapunguza kodi?” Alihoji.

Kulingana na sheikh Dor, serikali ina kazi kubwa ya kuhakikisha inaziba mianya ya ufisadi na ufujaji wa fedha za uma na kuelekeza fedha hizo kwenye utoaji huduma muhimu kwa Wakenya badala ya matozo ya juu ya ushuru ambayo hayamsaidii mkenya mlalahoi.

BY MAHMOOD MWANDUKA