HabariMichezoNewsSports

Msambweni 3 Wanyakua Ubingwa wa Dimba la Dola kaunti ya Kwale

Timu ya Msambweni 3 imenyakua ubingwa wa Dimba la Dola Super Cup Kaunti ya Kwale kwa kuinyuka Msambweni 2 mabao 4-0.

Kwenye ngarambi hiyo iliyosakatwa katika uga wa Maonyesho ya Ukunda imeshuhudia Msambweni 3 ikidhihirisha ubabe kupitia wachezaji Athman Bori aliyefunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya Hamidu Tabwara na Salim Mzara kuwahakikishia ushindi kwa kufunga bao la 3 na la 4 mtawalia kipindi cha pili.

Akizungumza baada mchuano huo, Saddam Suleiman Mkuu wa Mauzo wa Kampuni ya Dola amesema kuwa michuano hiyo imechipuza vipaji na kuwapa fursa vijana kaunti ya Kwale kudhihirisha talanta zao nchini na hata nje ya nchi.

“Tumepick players kwa kila bunge hapa kwa kuzingatia ubora na tumewapa nafasi wajikuze n talent zao zinaonekana hapa Kenya na outside Kenya since tuko na website ambayo inaangazia vipaji vyao. Kwale ni kubwa sana na we thank the county government imetusaidia sana logistics na mpango kuhakikisha wachezaji wanafika uwanjani on time.” Alisema.

Gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye alijitolea kuwazawidi washindi nyongeza ya pesa taslim shilingi elfu 30 katika zawadi ya laki moja waliopata, amesema kaunti ya Kwale inaboresha miundomsingi ya michezo na kwa sasa ujenzi wa Uwanja wa Kwale unakaribia kukamilika ili kukuza vipaji.

Gavana wa Kwale Fatuma Achani kwenye mashindano ya Dola Supercup katika uga wa maonyesho ya Ukunda

“Nashukuru sana kampuni ya Dola kwa kuleta tournament hii ikawaeka busy vijana na nafasi ya kukuza vipaji vyao. Kwale talent zipo na tunashirikiana pia tunakaribisha wawekezaji zaidi kuja kuchipuza vipaji. Tayari sisi tunakamilisha ujenzi wa Kwale stadium ambao uko hatua za mwisho kukamilika.” Alisema Achani.

Naye Mbunge wa Msambweni Feisal Bader amefichua kuwa awamu ya 3 ya mpango wa serikali wa ukuzaji talanta mashinani itatoa nafasi mwafaka kwa vijana kujiendeleza na kujipa ajira.

Fainali hiyo imevutia mashabiki wengi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali huku mshindi wa kipute hicho Msambweni 3 akitia kibindoni shilingi 100,000.

Msambweni 3 na mshindi wa pili Msamweni 2 sasa wamefuzu katika kipute cha mashindano hayo ya Dola makala ya Kaunti zote za Pwani ambapo zawadi kuu kwa bingwa atatia kibindoni shilingi Milioni moja.

BY MJOMBA RASHID