HabariNewsSiasa

ODM yafanya Mabadiliko; Viongozi wake Wakuu Walioteuliwa kuwa Mawaziri Wakijiuzulu Chamani

Chama cha ODM hatimaye kimetangaza mabadiliko mapya katika mfumo wake wa uongozi Bungeni kufuatia kuteuliwa kwa wanachama wake wakuu katika baraza la Mawaziri.

Chama hicho cha Chungwa kinachoongozwa na kinara wao Raila Odinga kimesema kimelazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya wanachama wake wanne walioteuliwa kuwa mawaziri kuwasilisha barua za kujiuzulu nyadhfa zao chamani sawia na majukumu yao ya awali ya bungeni.

ODM sasa imependekeza Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed kuchukua wadhfa wa Opiyo Wandayi kama Kiongozi wa Wachache Bungeni, naye Millie Odhiambo awe Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa wadhfa unaoshikiliwa na Junet.

Katika mabadailiko hayo pia ODM imependekeza Caleb Amisi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu Bungeni nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na John Mbadi, naye Wilberforce Oundo awe Naibu mwenyekiti wake.

Mabadiliko hayo yametangazwa leo na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari baada ya Kamati Kuu ya uongozi wa ODM kufanya mkutano na kinara wao Raila Odinga.

Ni rasmi Chama kimewaachilia viongozi wake ambao hivi majuzi waliteuliwa na Rais William Ruto kwa majukumu ya kitaifa kama Mawaziri. Nathibitisha kuwa nimepokea maombi ya kujiuzulu kwa John Mbadi kama Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, Opiyo Wandayi kama Katibu wa mausala ya Kisiasa ya ODM, kujiuzulu kwa Hassan Joho na Wycliff Oparanya kama Manaibu Vinara wa ODM, na Baetrice Askul Moe ambaye amejiuzulu kama mwanachama wa Kamati ya Uchaguzi katika ODM.” Taarifa ya Sifuna ilisema.

Ikumbukwe kuwa mnamo wiki iliyopita Rais William Ruto alimteua Mbunge wa Ugunja na KInara wa Wachache Bungeni James Opiyo Wandayi kuwa waziri wa Kawi, naye Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM John Mbadi akimpendekeza kushikilia Wizara ya Fedha.

Aidha Rais alimpendekeza Naibu Kinara wa ODM Hassan Joho kuwa Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini sawia na Naibu mwenza Wycliffe Oparanya aliyeteuliwa kushikilia Wizara ya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo Ndogo.

By Mjomba Rashid