LifestyleNewsSiasa

Waziri mpya wa Fedha Achukua Mikoba Rasmi, Aahidi Mageuzi na Kuimarisha Mapato ya Taifa

Waziri wa Hazina ya Kitaifa ya Fedha John Mbadi ameahidi kufanyia mageuzi zaidi katika hazina hiyo ikiwemo suala la mishahara ya wafanyakazi wa umma.

Mbadi amesema mikakati mizuri itawekwa kuhakikisha serikali inadhibiti changamoto za kiuchumi.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari katika Jumba la Hazina hiyo jijini Nairobi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi hiyo na Waziri mtangulizi wake Prof. Njuguna Ndung’u, Waziri huyo mpya wa fedha amewahakikishia wakenya kuwa serikali haitaurejesha mswada tata wa fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali.

Na Licha ya kuwa pigo serikalini kwa kupoteza mswada huo Mbadi amesema haitakuwa sahihi kuurejesha mswada huo na badala yake suala la matumzi ya ushuru unaokusanywa na mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA linapaswa kuangaziwa kwa jicho la Yakini.

“Ndio tulipoteza mswada wa fedha wa 2024 itakuwa ni makosa sana na matusi kwa Wakenya kuurejesha tena mswada huo, itakuwa ni kutowasilikiza Wakenya. Hivyo, hatuwezi kuurejesha mswada huo huo wa 2024 licha ya kuwa na vipengee muhimu vya kukuza Uchumi ndani yake, lakini nchi lazima ikue na isonge mbele.

Kuna vipengee vingepelekea nchi kukua, sehemu moja ni suala la matumizi ya kodi ambalo linapelekea kupotea kwa ushuru katika hilo, na tunajua kumekuwa na ukora lazima sasa tutafute njia za kupunguza matumizi ya ushuru,” alisema Mbadi.

Mbadi aidha alisema ni lazima Uchumi wa taifa uimarike akiwahimiza wakenya kukubaliana na mpango wa msamaha wa kodi huku akidokeza kuwepo kwa mifumo mizuri ambayo ikitumika itachangia taifa kuimarika zaidi kiuchumi, huku akiwasihi Wakenya kukumbatia kulipa ushuru badala ya kuhepa.

Wakati uo huo amefichua mipango na shughuli za wizara hiyo kuwekwa kwa umma ikiwemo kushirikishwa kwa wananchi katika vikao vya kutoa maoni ili kuchangia vilivyo kuimarika kwa mapato ya taifa.

Huyu hayo yakijiri, aliyekuwa waziri wa fedha Prof. Njuguna Ndung’u amefichua kuwepo kwa changamoto nyingi za kiuchumi nchini.

Akizungumza Jumatatu Agosti 12, baada ya kukabidhi rasmi afisi mrithi wake John Mbadi, Njuguna amesema kutopasishwa kumechangia ugumu wa kifedha nchini huku matumizi ya serikali yakiongezeka.

Kauli yake inajiri licha ya Serikali hivi majuzi kutangaza kupunguza matumizi yake na yale ya idara nyinginezo baada ya rais Ruto mnamo wiki jana kutia saini kuwa sheria mswada wa Nyongeza ya Ugavi, mswada unaopania kupunguza matumizi ya serikali kwa shilingi bilioni 145.7.

BY MJOMBA RASHID