HabariNews

Walimu Kupokea Nyongeza ya Mshahara wa Julai na Agosti Ijumaa hii

Serikali imetangaza nyongeza ya mishahara kwa walimu wote itakayoanza kutolewa Ijumaa hii.

Walimu wa shule za umma kote nchini watapewa nyongeza ya mishahara yao kuanzia mwezi Julai na Agosti.

Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba amesema tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 13.5 ili kutekeleza Mkataba wa Makubaliano wa mwaka 2021-2025 uliowapa walimu nyongeza hiyo, akiitaja hatua hiyo kuwa nia njema na kujitolea kwa serikali kuashughulia lalama za walimu.

Kama ushahidi wa nia njema na kujitolea kwa Serikali kushughulikia malalamishi ya walimu, Tume ya kuajiri Walimu, TSC imejitahidi vilivyo kuhakikisha kuwa walimu wote wa shule za umma wanalipwa nyongeza yao ya mshahara wa Julai na Agosti kufikia Ijumaa wiki hii (Agosti 30). Hii ni katika kutekeleza Mkataba wa Makubaliano, CBA ya mwaka 2021-25 baada ya Hazina ya Kitaifa ya Fedha kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 13.5.” alisema.

Ogamba ametangaza kuwa wanaendelea na mazungumzo na uongozi wa walimu wanachama wa KUPPET kushughulikia baadhi ya malalamishi yao ili kumaliza mgomo unaoendelea.

Wakati uo huo Waziri huyo amebaini kuwa serikali itaajiri walimu elfu 25 zaidi kufikia mwisho wa mwaka huu ili kukabiliana na uhaba wa walimu, huku akitoa hakikisho serikali inafanya juhudi zote kuhakikisha walimu 46,000 wa JSS wanapewa ajira za kudumu.

Ikumbukwe kuwa mnamo siku ya Jumapili Serikali ilikuwa imetoa shilingi bilioni 21.8 kwa shule zote za umma kabla ya ufunguzi rasmi wa shule kwa muhula wa tatu.

Elimu ya bure katika shule za msingi ikipigwa jeki kwa mgao wa shilingi bilioni 1.6, elimu ya bure kwa shule za Sekondari msingi ikipata shilingi bilioni 6.1 nayo elimu ya bure kwa shule za kutwa za upili ikipokea shilingi bilioni 14.1

Haya yanajiri huku mgomo wa walimu wanachama wa KUPPET ulionza siku ya Jumatatu kiendelea.

By Mjomba Rashid