HabariLifestyleNews

Afueni;Kaunti Kupokea Mgao wa Fedha Walizosubiria kwa Muda mrefu

Baada ya kipindi cha changamoto za kifedha kilichotokana na kucheweleshwa kwa mgao wa fedha kutoka serikali Kuu, hatimaye Serikali za Kaunti zinatarajiwa kupokea mgao wa fedha walizosubiria.

Hii ni kufuatia kikao muhimu kilichoandaliwa baina ya Baraza la Magavana, CoG na maafisa wa Hazina ya Kitaifa ya Fedha.

Waziri wa Fedha John Mbadi akiwa na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Ahmed Abdullahi pamoja na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wamekutana na kutatua tatizo lililopo la kuchelewa kwa mgao wa fedha za kaunti, tatizo lilokwamisha shughuli za maendeleo ya kaunti.

Waziri Mbadi amethibitisha kuwa majadiliano hayo yamezaa matokeo chanya na kaunti sasa zitarajie mgao wa fedha hizo hivi karibuni.

Ikumbukwe kuwa kaunti zimedai kutopokea fedha kwa kipindi cha miezi mitatu sasa hatua iliyopelekea kukwama kwa shughuli zake mbalimbali na miradi ya maendeleo ikiwemo kulipa mishahara wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine.

Kaunti zimelazimika kupambana na wakati mgumu hasa katika sekta ya afya ambapo huduma za matibabu katika hospitali za umma za baadhi ya kaunti zimelamaa kufuatia mgomo wa wahudumu wa afya, kaunti nyinginezo zikilazimika kutegemea mikopo ya wahisani na wawekezaji.

By Mjomba Rashid