HabariNews

Rais Ruto Amuidhinisha Kanja Kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi; Amsihi kuzingatia Sheria

Ni rasmi sasa Douglas Kanja ndiye Inspekta Jenerali mpya wa polisi baada ya kuapishwa kuchukua wadhfa wa Idara ya Polisi nchini, NPS.

Rais William Ruto amemteua Kanja kwa wadhfa huo baada ya bunge la Kitaifa kuidhinisha uteuzi wake siku ya Jumatano.

Akizungumza baada ya kuapishwa kwake katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amemtaka Kanja kuhakikisha kila Mkenya anatendewa haki na usawa kisheria pasi mapendeleo yoyote, sawia na kuhakikisha anailinda Idara dhidi ya hujuma zozote.

Katika kile kilichoonekana kumlenga Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli rais Ruto aidha amesisitiza kuwa chini ya uongozi wake Kanja ahakikishe kila moja nchini anaheshimu sheria za taifa hili pasi upendeleo wala kuzingatia nafasi aliyo nayo.

Bwana Kanja huku ukichukua mamlaka kama Inspekta Jenerali wa Polisi inakulazimu usimamie haki uilinde Idara hii kama taasisi huru dhidi ya hujuma na vitisho vyovyote. Uhakikishe kila raia anatendewa haki na usawa kisheria na hakuna aliye juu ya sheria. sote tuko viwango sawa mbele ya sheria,” alisema.

Douglas Kanja amechukua rasmi wadhfa huo wa Inspekta Jenerali wa Polisi ulioachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Japhet Koome mwezi Julai, sasa akisitisha Ukaimu wa Gilbert Masengeli.

Naye Masengeli anarejea kwenye jukumu lake la kuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi baada ya kukaimu majukumu ya wadhfa wa Inspekta Mkuuu wa Polisi kwa miezi kadhaa.

By Mjomba Rashid