HabariLifestyleNewsSiasa

Rais Ruto Avunja Kimya Chake na Kuahidi Kukomesha Visa vya Utekaji Nyara

Hatimaye Rais William Ruto amevunja ukimya wake kuhusu visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini na kuibua wasiwasi na kero.

Akizungumza mnamo Ijumaa katika uwanja wa Raila Odinga kaunti ya Homa Bay alikohudhuria fainali za kombe la Gavana, Rais Ruto ameahidi kukomesha visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini ili kuhakikisha taifa linakuwa na amani na utulivu.

Hata hivyo licha ya kutoligusia suala hilo kwa kina, katika kile kilichoonekana kuwalenga vijana waliobuni jumbe na vibonzo vya kejeli na ukosoaji mitandaoni, Rais amewasihi vijana kuzingatia nidhamu huku serikali ikiwajibikia visa vya utekaji nyara.

Wakati uo huo amewataka wazazi kuwajibikia majukumu yao na kuwachunga watoto wao dhidi ya mienendo potofu.

Na yale yamesemekana mambo ya abduction tutakomesha ndio vijana wa Kenya waweze kuishi kwa amani na vilevile wawe na nidhamu ili tuweze kujenga Kenya pamoja.” Alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, aliyekuwa Waziri Mkuu na ambaye pia ni mgombea wa Uenyekiti wa Tume ya Afrika AUC, Raila Odinga amekariri kuwa visa vya utekaji nyara vinapaswa kukomeshwa, akimtaka Rais Ruto kushughulikia suala hilo kwa haraka na kuhakikisha waliohusikana na visa hivyo wanakabiliwa kisheria.

By Mjomba Rashid