HabariNews

Rais Ruto Atangaza Wakenya Wote Wapewe Vitambulisho vya Kitaifa Bure

Rais William Ruto sasa ametangaza kuwa Wakenya wote wapewe vitambulisho vya kitaifa bila gharama yoyote.

Hii ni licha ya serikali awali kudokeza nia ya kuongeza malipo ya kupata stakabadhi hiyo muhimu hadi shilingi 2,000 kabla ya notisi ya gazeti la serikali iliyotolewa Novemba 7, 2023, kubatilishwa.

Akizungumza alipokuwa kwenye ziara katika mtaa wa mabanda wa Kibra jijini Nairobi anakoendeleza ziara, rais pia amesema atakomesha unyanyasaji, ubaguzi na upendeleo unaozingira utoaji wa vitambulisho.

“Nimesema maneno ya ubaguzi kwa mambo ya ID tuyatupilie mbali; kila mwananchi apatiwe ID. Natangaza nikiwa hapa Kibra ya kwamba kitambulisho ipatianwe bila malipo yoyote.

Kila mtu apatiwe kitambulisho bila malipo na kwa mpango ambao hauna ubaguzi kwa Wakenya,” akasema Rais.

Serikali ilikuwa na nia ya kuongeza ada ya kutuma maombi ya vitambulisho kwa mara ya kwanza hadi shilingi 1,000 lakini ikakagua gharama hiyo kushuka hadi shilingi 300.

Ada ya kubadilisha vitambulisho vilivyopotea pia ilipunguzwa hadi shilingi 1,000 kutoka shilingi 2,000 iliyokusudiwa.

Kauli ya Rais Ruto inajiri kufuatia hatua yake ya hivi majuzi yenye utata ya kufutilia mbali matakwa ya miaka 60 ya uhakiki kwa waliotuma maombi ya vitambulisho vya kaunti za mpakani.

By Mjomba Rashid