Serikali imetenga shilingi bilioni 2.5 katika bajeti ya ziada kupiga jeki mpango wa kulinda amani wa nchini Haiti.
Katika bajeti ya ziada iliyo mbele ya Bunge la Kitaifa kwa sasa, Kamati ya Uhusiano imekubali ombi la serikali ya kitaifa kama sehemu ya shilingi bilioni 23 zilizotolewa kwa sekta ya usalama.
“Sekta ya usalama imetengewa shilingi bilioni 7.5 za ziada kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, ambapo shilingi bilioni 5 ni kushughulikia upungufu wa gharama za bima na shilingi bilioni 2.5 kusaidia misheni ya kulinda amani ya Haiti,” ilisoma sehemu ya ripoti hiyo.
Licha ya serikali kusisitiza kuwa ujumbe wa Haiti hautafadhiliwa na pesa za walipa kodi, hii ni mara ya pili inatafuta pesa kusaidia misheni hiyo.
Hapo awali, serikali ilikuwa imetafuta shilingi bilioni 2.1 kusaidia ujumbe wa kulinda amani, huku Waziri wa Fedha akieleza kuwa pesa hizo zingerejeshwa na UN.
Hadi kufikia sasa fedha zilizotumika katika mpango huo wa kulinda amani katika nchi hiyo ya visiwa vya Carribean zimefikia shilingi bilioni 4.9.
Tangu maafisa wa polisi walipoondoka nchini kwenda huko Haiti ni muda wa miezi 9 kwa sasa.
By Mjomba Rashid