HabariNews

Ubabe wa Kisiasa kati ya Sarai na Jicho Pevu Watikisa Hafla ya Rais Mombasa, Rais Akisistiza Umoja

Rais William Ruto amewataka wanasiasa kusitisha ubabe na mashindano ya kutafuta umaarufu na badala yake kuangazia masuala yanayowahusu Wakenya.

Akizungumza hapa mjini Mombasa mnamo Jumatatu Julai 29 katika hafla ya ufunguzi wa Shule ya Walio na Ulemavu wa Akili Pwani huko eneobunge la Nyali Rais Ruto aliwataka viongozi kukumbatia umoja na kazi ya pamoja ili kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi.

Alisisitiza kuwa licha ya kutoka katika mirengo tofauti ya kisiasa, viongozi wanatakiwa kuweka masilahi ya nchi mbele kuliko maslahi yao binafsi.

“Lazima tuweke umoja wa nchi na masilahi ya Wakenya mbele na sio yetu kama viongozi,” alisema.

Wakati uo huo Rais alilazimika kuingilia kati kutuliza uhasama na ubabe wa kisiasa kutawala hafla yake hiyo.

Ni baada ya Mbunge wa Nyali Mohammed Ali kuoneshana ubabe na kurushiana cheche za maneno na Naibu Mwenyekiti wa UDA aliye pia Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki EALA, Hassan Omar Sarai.

“Noana hapa kidogo kuna ubabe wa kisiasa, mimi nawaomba tafadhali ndugu zangu, ndugu yangu Hassan Sarai ndugu yangu mdogo Mohammed Ali nawaomba viongozi pia pande zote ya, upande wetu wa UDA na upande wa ODM nawaomba sasa tuwache ubabe chini tuungane tuweze kupeleka Mombasa, Pwani na Kenya mbele.” Alisema.

Rais alizungumza hayo wakati wa ufunguzi wa shule ya Pwani kwa Walio na Ulemavu wa Akili na uwekaji wa jiwe la msingi la Chuo cha Mafunzo ya Ufundi ya Nyali (TVET) huko Nyali, Kaunti ya Mombasa.

Haya yamejiri baada ya 2 hao kurushiana maneno walipokuwa wakihutubia wakaazi katikahafla hiyo.

Ruto aliwashauri wawili hao ambao tayari wametangaza azma ya kuwania wadhifa wa ugavana kaunti ya Mombasa kwenye uchaguzi mkuu ujao kuzingatia Umoja.

By Mjomba Rashid