HabariNews

Waziri Mteule wa Mazingira Aapa Kukabiliana na Unyakuzi wa Ardhi za Misitu Atakapoidhinishwa

Waziri mteule wa Mazingira Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi Adan Bare Duale ameapa kupambana na mabwenyenye wanyakuzi wa ardhi za misitu kwa muda wa siku 30 iwapo ataidhinishwa na Bunge.

Akiwa mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi mnamo Ijumaa Agosti 2, Duale alisema atabatilisha hatimiliki za ardhi za hifadhi ya misitu alizodai kumilikiwa na baadhi ya wakuu fulani Serikalini.

Bila hofu ya kwenda kinyume nasema kuwa Bunge hili likiniidhinisha siku 30 za kwanza nikishirikiana na Waziri wa Ardhi na idara nyingine za Kiserikali nitabatilisha hatimiliki kadhaa zikiwemo zile za watu wakuu serikalini, baadhi yake zikiwemo zile za baadhi ya Wabunge.” Alisema.

Japo hakufichua majina, Duale alisema yu tayari kwa lolote litakalomtokea atakapochukua hatua hiyo hasa baada ya kusema kuwa kuna watu mashuhuri walio na ushawishi serikalini wanamiliki ardhi zilizo na hifadhi ya misitu ikiwemo Msitu wa Ololua.

Niko tayari kwa matokeo yoyote kwa hatua nitakayochukua kuhusiana na hilo.

Na kwa suala lile la Ololua nimepewa habari na nimesikiza kwa wataalum na nasema inaskitisha kuwa kwa miaka miwili iliyopita kuna watu walipata hatimiliki haramu.” Alisema Duale.

Aidha Duale amesema suala la ufisadi katika sekta mbalimbali ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa kuliko hata tishio la wanamgambo wa Alshabab.

Duale ameeleza kuwa muhimu ni kukomesha ufisadi unaondelea katika taasisi na idara za Wizara ya Mazingira na misitu ambayo imedumu kwa muda mrefu bila suluhu.

Kuhusiana na suala la usajili wa makurutu alipokuwa Waziri wa Ulinzi Duale amesema sheria za usajili wa makurutu kujiunga na jeshi ni tofauti na sheria za usajili wa maafisa wa polisi na hata wa misitu.

By Mjomba Rashid