HabariNews

Ugonjwa wa nasuri wahusishwa na ushirikina Viragoni, kaunti ya Kilifi

Wakazi wa Viragoni eneo bunge la Kaloleni, wanahusisha ugonjwa wa nasuri maarufu fistula na ushirikina, hali hii ikisababisha wanawake wengi wanaougua nasuri kuathirika zaidi kwa kukosa matibabu hospitalini.

Nasuri ni ugonjwa unaosababisha kuvuja mkojo au kinyesi kwa wanawake, mara nyingi ugonjwa huu hutokea wakati wa wanawake wajawazito wanapoumwa na uchungu wakutaka kujifungua kwa muda mrefu bila kupata huduma za uzazi.

Sophia Kalume daktari wa nyanjani wadi ya Kayafungo, anasema wanawake wengi wamekuwa wakipitia changamoto ya afya kutokana na ugonjwa huo wa nasuri ambao baadhi ya wakazi wa kijiji cha Viragoni eneo bunge la Kaloleni wanaamini kuwa ugonjwa wa nasuri unatokana na uchawi.

Anasema baadhi ya wakazi hao wamekosa ufahamu kuhusu ugonjwa huo, jambo linalowafanya kuwaficha waathiriwa wa ugonjwa wa nasuri na kusababishia kuumia zaidi.

“Hata kuna kisa kimoja nilipigiwa simu na chifu wa kata ya Viragoni akanambia kuna kesi hapa niliiskiliza juzi kuna mama ambaye ana hali kama hizo ambazo unasaidia kina mama lakini wanawe wana imani za kichawi wanaamini kwamba mama yao anarogwa.

“Kwa hivyo nikawaambia ikiwa huyu mama tatizo ni hilo atasaidika. Kwa sababu ule ugonjwa ulikuwa umekaa sana mpaka akili ya yule mama ikawa haifanyi kazi vizuri. Hapo nikaongea na mwanawe wa kiume akakubali mamake apate usaidizi wa matibabu.

“Tukamtanguliza kwa mshauri kwanza halafu tukampeleka kwa madaktari wa kutibu nasuri na hakika yule mama akasaidika.” alisema Sophia.

Aidha amesema kupitia hamasa ya mara kwa mara kwa wakazi, dhana hiyo potofu kutoka kwa wakazi imeanza kusahaulika.

Ameeleza kuwa kuna hatua kubwa ambayo imepigwa katika kukabiliana na ugonjwa wa nasuri kaunti ya Kilifi kufuatia madaktari waliopata mafunzo ya kukabiliana na ugonjwa wa nasuri kuwekwa katika vituo vya afya vinavyopeana huduma ya uzazi.

Kwa sasa tunakuta kwamba dhana hizi potofu zinaendelea kupungua kwa sababu wengi tunawaelimisha na madaktari wengi kwenye vituo vya afya vinavyotoa huduma za uzazi wamepata mafunzo ya kushughulikia ugonjwa huu wa nasuri mfano Mariakani, Kilifi na Malindi kuna madaktari maalum wakushughulikia nasuri.” alisema Sophia.

Erickson Kadzeha