HabariNewsUncategorized

Mkurugenzi wa MUHURI Khelef Khalifa Akamatwa na Maafisa wa Polisi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI, Khelef Khalifa amekamatwa na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi eneo la Mida, Malindi Kaunti ya Kilifi.

Afisa wa Masuala ya dharura Francis Auma amethibitisha hilo akidai kuwa Khalifa alikamatwa mapema leo Jumamosi akiwa katika gari lake na familia yake akielekea Malindi.

Auma amedai kuwa juhudi za kumtafuta kule alikozuiliwa zinaendelea akisema maisha ya Mkuu wao huyo huenda yakawa hatarini.

Afisa huyo wa MUHURI, amedai kuwa kukamatwa Kwa Khalifa huenda kunatokona na juhudi zake za kupigania uongozi bora nchini ambapo mara Kwa mara ameikosoa serikali kila inapopoteza dira ya uongozi.

“Tunajua Khelef amekuwa vocal sana on government akichampion good governance akipigania haki na amekuwa mstari wa mbele sana. Nasema wamemkamata as we speak na hatujui wamempeleka wapi.” Alisema Auma.

Aidha ripoti zinaarifu kuwa Khelef alikamatwa alipowauliza maafisa wa usalama waliokuwa kwenye kizuizi cha barabarani eneo hilo la Mida sababu ya kuficha nyuso zao licha ya agizo la mahakama la hivi majuzi kutaka wasifche sura zao wanapokuwa kwenye oparesheni hasa za maandamano.

Tume ya Kutetea haki za kibinadamu nchini KHRC kwenye taarifa yake katika mtandao wake wa X imeshinikiza idara ya usalama kumwachilia mara moja Khalifa, ikisema kuwa alikuwa sawa kisheria kutaka maafisa hao wajitambulishe kwa kuweka nyuso zao wazi.

“Kisheria alikuwa sawa kuwataka wajitambulishe, na sasa uhuru wake unatishiwa. Tunashinikiza Khalifa na familia yake waachiliwe mara moja.” Ilisema taarifa yake.

Hata hivyo Khelef baadaye aliachiliwa baada ya saa zaidi ya nne tangu alipokamatwa.

Akieleza yaliyojiri, Khelef amedai kuachiliwa kwa bondi ya shilingi  10,000 baada ya kuandikiwa makosa ya kufanya usumbufu, japo akasema kuwa atawasilisha kesi kortini kuhusiana na yaliyotokea.

“Baada ya kuwambia wajitambulishe watoe sura zao na nembo rasmi ya majina kwenye sare zao, walikataa wakasema wao ni special force. Nikasema hapa lazima mjitambulishe kisheria. ndio wakaniweka kando tangu asubuhi hadi saa nane baadaye wakanipelekea kituoni Malindi walikoniandikia makosa hayo. Nasema hatuezi kuliwacha hivi, lazima hii kesi iendelee.” Alisema.

itakumbukwa kuwa Mahakama Kuu mnamo wiki jana ilipia marufuku maafisa wa polisi kuficha nyuso zao wanapokuwa katika oparesheni zao na hata kumwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi kuhakikisha maafisa wa polisi wanajitambulisha wakati wa maandamano.

BY NEWS DESK