HabariNews

13 Wafariki katika Ajali iliyohusisha Basi la Coast Bus eneo la Migaa, Salgaa barabara ya Eldoret-Nakuru

Watu 13 sasa wamethibitishwa kufariki Katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea eneo la Migaa karibu na Salgaa katika barabara kuu ya Eldoret-Nakuru.

Idadi hiyo imeongezeka baada ya miili mitano zaidi kutolewa kwenye mabaki ya basi walilokuwa wakisafiria.

Ajali hiyo iliyotokea saa kumi alfajiri ya Jumanne Agosti 20, ilihusisha basi la kampuni ya Coast Bus lililokuwa likitoka Kakamega likielekea mjini Mombasa na gari dogo la abiria lililokuwa likitokea Nakuru.

Kulingana na manusura wa ajali hiyo basi hilo linadaiwa kukumbwa na hitilafu za kimitambo likiwa Kericho kabla ya kuonekana kupoteza breki na kugongana na gari dogo la kibinafsi.

Tumepigiwa simu tukakuja hapa tukakuta Coast bus iligonga ile gari ndogo na kuanguka hapa. Tunaambiwa kwamba na abiria hii gari ilikuwa imeharibika wakaripoti Kericho gari haikuwa nzuri lakini hawakusikika na wakakuja hadi ikatokea hapa.” Alisema mmoja wa waliofika kuwanusuru.

11 kati ya waliofariki walikuwa abiria wa basi hilo na wawili abiria wa gari dogo hilo la kibinafsi.

Kamanda wa polisi eneo la Bonde la Ufa Jasper Ombati amesema abiria wengine 55 walipata majeraha na wanaendelea kutibiwa katika hospitali mbalimbali eneo hilo.

Shughuli za uokozi zimeendelea mapema Jumanne asubuhi huku Shirika la Msalaba Mwekundu nalo likibaini kuwa watu 36 walikuwa wakitibiwa katika hospitali za Coptic na Molo.

By Mjomba Rashid