HabariNews

Walimu wa shule za upili zaidi ya 3,000 washiriki mgomo Kilifi

Shule zikifunguliwa kwa muhula wa tatu kote nchini, walimu zaidi ya 3,000 wanaoshiriki mgomo wameapa kutorudi kazini hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa na tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC. Na sasa walimu hao wametoa onyo kwa wazazi kutowapeleka watoto wao shuleni kwani hakutakuwa na walimu shuleni.

Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kati nchini KUPPET kaunti ya Kilifi kimeapa kutowaruhusu wanachama wake kurudi shuleni hadi pale tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC itakapotimiza matakwa yao 10.

Katibu wa KUPPET kaunti ya Kilifi Caleb Mogere amaesema TSC imefeli kutekeleza makubaliano ya awali ambapo walimu zaidi ya 130,000 wa ngazi tofauti tofauti wanafaa kupandishwa vyeo.

 

“Walimu wamekwama kwenye kiwango fulani cha kazi kwa zaidi ya miaka 20, tunataka walimu 130,000 wapandishwe vyeo na wale elfu 46 wa sekondari msingi waajiriwe kwa misingi ya kudumu haraka iwezekanavyo kama si hivyo basin a sisi hatutarudi madarasani.” alisema Mogere.

 

Ametoa wito kwa wazazi kusalia na watoto wao nyumbani kwani walimu hawatakuwepo shuleni, huku akiwaonya wakuu wa shule wanaowashurutisha walimu kuendelea na majukumu yao kukoma mara moja.

Aidha ameutaja muungano wa kitaifa wa walimu KNUT unao endelea na shughuli za masomo kuwa unawapotosha wazazi.

Shirika lolote lile linalodanganya wazazi wapeleke watoto shule hata KNUT tunataka kuwaambia hivi kule shuleni hakuna walimu. Walimu wote tuko hapa tunaandamana tuko barabarani wanaendeleza mchakato wa kuboresha alama ya idadi jumla wakiwa nyumbani hawako shuleni kwa hivyo wazazi tunawaomba msipeleke watoto wenu shuleni.” alisema Mogere.

 

Chiguba Morris Nyale mwenyekiti wa chama cha KUPPET kaunti ya Kilifi amesema TSC imefeli kutekeleza makubaliano tangu mwezi Julai akitaja hatua hiyo kuwa unyanyasaji wa walimu.

Ameongeza kuwa walimu hawatatishwa na TSC na hivyo basi kuapa kutorudi madarasani mpaka pale matakwa yao yatakapotimizwa.

 

Leo ni ile siku ambayo tulikuwa tumeahidiana na mwajiri wetu TSC kwamba wasipotimiza yale matakwa ya walimu sisi hatutarudi madarasani.Kuna mambo tulikubaliana pale makubaliano yao yatekelezwe kikamilifu kuanzia tarehe moja Julai na mpaka sasa hivi hayo hayajatimizika.Lakini tunataka kusema kwamba hatutatishwa na mwajiri wetu kwasababu sisi ndio watoaji wa huduma.”  alisema Chiguba.

 

Mae Kitsao Ngowa mweka hazina wa chama hicho cha KUPPET kaunti ya Kilifi ameeleza kuwa manaibu wa walimu wakuu wamedhulumika kwa kukosa nafasi ya kusimamia shule licha ya kuwa na vigezo vya kutosha kwa madai ya TSC kufuata muogozo wa muendelezo wa taaluma CPG.

Naibu walimu wakuu wakifika kiwango cha C4 wanatosha kabisa kusimamia shule kama vile zamani tulivyokuwa tukiita M. Yeye anatosha kusimamia shule na sasa manaibu walimu wakuu wengi na wasimamizi wa taasisi wamekwama kwasababu ya muogozo wa muendelezo wa taaluma “career progressive guidelines” CPG. Hiyo tumeikataa na walimu wamekataa” alisema Ngowa.

 

Erickson Kadzeha