HabariNews

Gilbert Masengeli Ahukumiwa Miezi 6 Jela

Hatua ya Kaimu inspekta Jenerali wa polisi nchini Gilbert Masengeli kupuuza magizo ya mahakama mara 6 licha ya kuamrishwa kufika mahakamani na jaji Lawrence Mugambi inafaa ikashifiwe na kukemewa zaidi.

Kwanza, ishutumiwe Kwa sababu mienendo yake Masengeli haifai hata kidogo sio tu kwake bali pia kwa afisa yeyote anayeshikilia ofisi ya umma nchini kuendeleza hulka kama hiyo. Pili, iwapo mienendo yake Masengeli ingeigwa na kila mtu nchini huenda hali hiyo ikalitumbikiza taifa kwenye lindi hatari; lindi la madharau dhidi ya majaji na mapuuza Kwa mahakama na sheria za nchi kwa jumla.

Gilbert Masengeli Kwa sasa ni mfano mbaya sio tu kwa wakubwa na wadogo wake ndani ya idara na asasi zote za usalama nchini bali pia machoni pa Raia .Ni mfano hai wa kiongozi aliyelewa mamlaka kupita kiasi na sasa anahujumu sheria kwa kukiuka na kubaka kila Kipengee cha Katiba na ibara zote za katiba ya nchi pasi kuhofia lolote.

Kutofika Kwake Mahakamani mbele ya jaji Lawrence Mugambi licha ya jaji huyo kutoa amri Masengeli afike mwenyewe kuweka wazi anachojua kuhusu kupotea kwa mwanaharakati Bob Robert Njagi anayedaiwa kutekwa nyara na maafisa wa Polisi akiwa katika barabara kuu ya Mombasa akielekea Mlolongo na ndugu wawili Jamil Longton na Aslam Longton eneo la kitengela Agosti 19 mwaka huu walipokuwa wakielekea Kiserian inaarishia Kaimu inspekta huyo mkuu wa polisi anajua mengi ambayo wakenya hawayafahamu na sasa ana kila sababu ya kuogopa kupasua mbarika.

Alipokuwa akitafutwa na Mahakama mjini Nairobi wiki jana alijifanya ana majukumu mengi ya kikazi mjini Mombasa na Wajir, ilhali awali alionekana akipunga unyunyu kisiwani Mombasa ndani ya mkahawa wa Pride Inn Paradise Shanzu, mjini Mombasa kabla ya kuondoka siku chache baadae. Pili , hatua yake ya kumtuma Kaimu wake David Lagat kumwakilisha mahakamani inaashiria Masengeli anadunisha mahakama maksudi na kuwadharau majaji waliotwikwa jukumu la kikatiba kuwasikiliza wakubwa kwa wadogo ili kutoa hukumu Kwa kila mmoja. Tatu, sababu zilizotolewa na wakili wa serikali Charles Mutinda hazina msingi wala mashiko maana zilionekana wazi kuwa vijisababu tu.

Kilichowazi ni kwamba,Masengeli anakwepa maksudi kuzungumzia kuhusu kutekwa nyara kwa watatu hao wanaodaiwa kutekwa na maafisa wa polisi ambao lau kama si amri yake wasingetekeleza kamatakamata hiyo ya kiholela. Maji yamezidi unga na sasa inamuwia vigumu kuelezea jinsi gani wakenya wasio na hatia wanatekwa nyara na maafisa wa Polisi ambao wanafaa kuwalinda pasi kudhulumu hazi zao.

Rais William Ruto alipokuwa Mjini Kisumu alijitia hamnazo peupe mbele ya Kamera na kusema kuwa hana ufahamu wala hajui jina la mkenya yeyote ambaye amepotea Kwa njia ya kutekwa nyara. Mheshimiwa Rais William Ruto; Bob Njagi, Jamil Longton, Aslam Longton, Gideon Muli wote wanadaiwa kutekwa nyara eneo la Kitengela Agosti 19 mwaka huu na hadi kufikia sasa hawajulikani walipo. Purity Njeri ni mkenya mwengine ambaye amepotea Kuanzia 11 Julai mwaka sawia na Emmanuel Kamau aliyepotea kwenye Mazingira tatanishi Nairobi CBD Juni 25 na ambaye ametafutwa kwa udi na uvumba ila hapatikani.

Lilian Moseti pia alipotea huko Ruiru nao Kirui Chebet, Jombatech Mattos walioonekana mara ya mwisho huko Baringo wote wakipotea katika mazingira tatanishi na licha ya kutafutwa hawapatikani.Owino Evance Onyiego aliyeonekana mara ya mwisho Kitengela hapatikani,naye Joseph Otieno pia hajulikani alipo kwa sasa tangu kuonekana mara ya mwisho karibu na majengo ya Bunge.

Emmanuel Kamau Mukuria ni mkenya mwengine ambaye amepotea na mara ya mwisho kuonekana alikuwa Katikati mwa jiji la Nairobi 9 Julai naye Peter Macharia pia akitoweka alipokuwa barabara ya Ngong maeneo ya Jamhuri.

Majina ya watatu hao ambao ni Bob Robert Njagi, Aslam Longton na Jamil Longton yanamtia kisunzi Gilbert Masengeli, hata ndotoni anaogopa hata kuwa na uoga kuelezea mahali walipo watu hawa wasio na hatia, na iwapo wanayo hatia inamuwia vigumu kuelezea mbona hawajafikishwa Mahakamani saa 24 zaidi tangu kukamatwa kwao.

Ijumaa ya septemba 13 mwaka huu, jaji wa mahakama Kuu Lawrence Mugambi anatarajiwa kutoa hukumu dhidi ya Masengeli. Hebu niseme hivi, sheria inafaa ifuate mkondo wake angaa Masengeli atumike Kama mfano kwa viongozi wengine waliolewa mamlaka na kumea Pembe kama Masengeli.

BY ISAIAH MUTHENGI