AfyaHabari

Rais apiga marufuku kuingia na kutoka kaunti tano humu nchini….

Rais Uhuru Kenyatta amepiga marufuku usafiri wa kuingia na kutoka katika kaunti za Nairobi, Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru kuanzia leo saa sita usiku huku marufuku ya kutotoka nje usiku maarufu kafyu kwenye kaunti hizo tano sasa ikitarajiwa kuanza saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri.

Hii ni baada ya kaunti hizo tano kuendelea kuandikisha idadi ya juu ya maambukizi, huku idadi ya vifo kutokana na corona pia ikiendelea kuongezeka.

Akizungumza katika ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta amesema shughuli za ibada katika kanisa na misikiti kaunti hizo zimefungwa kuanzia leo usiku ili kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Rais Kenyatta aidha amepiga marufuku mikutano ya hadhara katika kaunti hizo tano akisem mikutano hiyo inapaswa kuhudhuriwa na wati 15 pekee.

Wakati huo huo rais Kenyatta ameamuru shule zote na taasisi za elimu na vyuo kwenye kaunti hizo kufungwa haraka iwezenavyo.

Anasema wanafunzi wanaofanya mtihani wa KCSE pekee ndio wataendelea na mtihani hiyo.

Uhuru anasema tangu alipohutubia taifa tarehe 12 ya mwezi huu, wakenya 7,630 wamelazwa katika hospitali mbali mbali wakiwa na covid 19 huku kiwango cha wagonjwa wanaolazwa kikiongezeka hadi asilimia 52.

Hata hivyo masharti ya kudhibiti maambukizi katika kaunti zilizosalia yatasalia kama ilivyokuwa huku wananchi wa kaunti hizo wakionywa kuwa makini zaidi.

Hatua ya rais Kenyatta ya kufunga kaunti hizo imekosolewa vibaya haswa kwa waumini wa dini ya kiislamu ambao wanatarajiwa kuanza mfungo wa mwezi mtukufu.