Jaji wa mahakama kuu Said Juma Chitembwe ameitetea azma yake ya kutaka kuwa jaji mkuu.
Akiwa mbele ya makamishna tisa wa tume ya huduma za mahakama JSC ikiongozwa na mwenyekiti Olive Mugenda, Chitembewe ameanza kwa kujieleza kuhusu masomo yake huku akisema anaendeleza kazi iliyoachwa na majaji watangulizi wake ambao ni Willy Mutunga na David Maraga akisema anazifahamu vyema changamoto zinazoikumba sekta ya mahakama.
Chitembwe amejitetea kutokana na uzoefu wake katika idara ya mahakama akisema anafahamu vyema majukumu ya jaji mkuu.
Chitembwe aidha amekabiliwa na wakati mgumu kuwaeleza makamishna wa JSC wanaoendeleza mchujo huo jinsi atakavyoimarisha uhusiano wa serikali ya utendaji na idara ya mahakama.
Kamishna Mohammed Warsame ambaye pia ni jaji wa mahakama ya rufaa amemtaka jaji Chitembwe kufafanua jinsi atakavyoshughulikia hatua ya rais Uhuru Kenyatta ya kukataa kuwaidhinisha majaji 41 waliopendekezwa na tume ya huduma za mahakama.
Katika jibu lake, Chitembwe amesema atafuata utaratibu kumueleza rais Uhuru Kenyatta kuhusu umuhimu wa kuidhinishwa kwa majaji hao ili kukabili mrundiko wa kesi mahakamani.
Alipoulizwa atatumia njia gani kuhakikisha maagizo ya mahakama yanaheshimiwa na kutekelezwa, Chitembwe amesema atatumia mfumo wa majadiliano ili kuhakikisho maagizo ya mahakama yanafuatwa.
Hapo kesho Profesa Kameri Mbote atakutana na tume hiyo, ilhali jaji Martha Koome atahojiwa siku ya Jumatano.
Jaji Marete Njagi na wakili Philip Murgor watafika mbele ya jopo hilo Alhamisi na Ijumaa mtawalia.
Wawaniaji wengine watano watasailiwa juma lijalo kwenye shughuli hiyo inayotarajiwa kuchukua siku kumi.