Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewasili nchini kwa ziara ya siku mbili.
Rais Suluhu ambaye ameandamana na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu miongoni mwa wajumbe wengine, amepokelewa na waziri wa maswala ya kigeni nchini Raychelle Omamo katika uwanja wa ndege wa JKIA.
Rais Uhuru Kenyatta na Rais Suluhu wanatarajiwa kuhutubia taifa baada ya mazungumzo ya faragha.
Baadhi ya maswala ambayo yanatarajiwa kuzungumziwa ni nafasi za kibiashara, uwekezaji na mikwaruzano ya kibiashara, ziara hii ikitarajiwa kuboresha mahusiano baina ya mataifa haya mawili.
Rais Suluhu aidha anatarajiwa kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge na seneti hapo kesho.
Aidha, Rais Suluhu atahudhuria na kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania utakaofanyika jijini Nairobi.
Alifanya safari yake ya kwanza akiwa Rais nchini Uganda mnamo Aprili 11 na Rais Yoweri Museveni akielezea kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kumaliza makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka nchini Uganda.
Rais huyo ameonekana kutopendelea kulinganishwa na Magufuli na amewashutumu wabunge wa Tanzania kwa kufanya hivyo.