Serikali ya kaunti ya Kwale haijapokea zaidi ya shilingi bilioni 2.7 ambazo ni fedha za matumizi za mwaka wa kifedha wa 2020/2021.
Kulingana na waziri wa fedha kaunti ya Kwale Bakari Sebe, serikali ya kaunti hiyo haijapokea fedha hizo tangu mwezi Machi mwaka huu.
Akizungumza katika eneo la Kinondo, Sebe ameitaka serikali kuu kuhakikisha inatoa fedha hizo kwa wakati ili waweze kulipa madeni na mishahara ya wafanyikazi.
Waziri huyo amesema kuchelewesha kwa fedha hizo kumechangiwa pakubwa na janga la corona ambalo limeathiri pakubwa uchumi wa taifa.
Sebe ameitaka serikali ya kitaifa kuharakisha utoaji wa fedha hizo baada ya janga hilo kuathiri ushuru unaokusanywa kaunti ya Kwale.