Wakaazi takriban 1600 kutoka eneo bunge la Samburu ambao wameathirika na ukame wamepokea chakula cha msaada kutoka kwa kampuni ya uchimbaji madini ya Base Titanium kama njia ya kukabiliana na janga la njaa sehemu hiyo.
Hii ni baada ya wakaazi wa Mwembeni katika eneo bunge hilo la Samburu walioachwa bila makao baada ya nyumba zao kuchomwa na watu wasiojulikana wiki iliyopita kuomba msaada wa chakula kutoka kwa serikali ya kaunti.
Akizungumza wakati wa kupeana chakula hicho mkurugenzi wa miradi ya jamii katika kampuni hiyo Mwanaharusi Hamisi amedokeza kuwa chakula hicho kimegharimu shilingi million 6 na wao kama kampuni wanashirikiana pamoja na serikali ya kaunti ya Kwale ili kusaidia familia ambazo zimeathirika Zaidi na baa la njaa.
Ali Ngombeko ni mmoja wa wakaazi waliopokea msaada huo na ameipongeza kampuni hiyo ya madini pamoja na serikali ya gatuzi katika hatua zake za kukabiliana na ukame.
Kati ya vijiji ambavyo vimepokea chakula hicho ni pamoja na Chigutu, Vinyunduni, Ryakalui, Kizingo na Mwanagza pamoja na wakaazi wa Mwembeni eneo la Samburu waliovunjiwa makaazi yao juma lililopita.
BY EDITORIAL DESK