HabariNews

TAKRIBAN WAKULIMA ELFU 98 WASAJILIWA KUPATA MBOLEA YA BEI NAFUU KILIFI.

Takriban wakulima elfu 98 wamesajiliwa kupata mbolea ya bei nafuu kaunti ya Kilifi, huku wito ukiendelea kutolewa kwa wakulima kuendelea kujisajili.

Kufuatia kushuhudiwa kwa uhaba wa chakula nchini hususan mahindi kulikochangia kupanda kwa bei za vyakula, serikali ya kitaifa ilianzisha mpango wa kukabiliana na changamoto hii ya uhaba wa chakula nchini kwa kuahidi kugawanya mbolea ya bei nafuu kwa wakulima kote nchini.

Kwa mujibu wa kaimu kamishna wa kaunti hii ya Kilifi Geofrey Tanui, mpango huo ukiendelea kote nchini, sasa anasema wakulima kaunti hii ya Kilifi wamehimizwa kuendelea kujisajili ili waweze kupata mbolea hiyo ya bei nafuu pamoja na kutayarisha mashamba yao ili mvua zitakapoanza kunyesha upanzi uanze mara moja.

Aidha amewataka wakulima walio na wasi wasi wa kutumia mbolea katika mashamba yao kwa hofu ya kuharibu mchanga kuondoa hofu hiyo kwani mbolea hiyo imepasishwa na serikali, huku akiongeza kuwa wakulima wengi hapa kaunti ya Kilifi hawajanufaika vilivyo na kilimo kwa ukosefu wa kutumia mbolea.

BY ERICKSON KADZEHA