HabariNews

MASHIRIKA YA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU YATAKA MAPENDEKEZO YA MSWAADA WA FEDHA 2023 KUTOPITISHWA

Mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu zimewataka wabunge kutopitisha mapendekezo ya mswaada wa fedha 2023, kwa madai kuwa mswaada huo, utazidisha ugumu wa maisha kwa wananchi.

Hisia mseto zinaendelea kutolewa dhidi ya mswaada wa fedha 2023 unaopendekezwa na serikali, kutokana na kile kinachotajwa kuwa mswaada huo utazidisha gharama za maisha.

Kwa mujibu wa Julius Wanyama afisa kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la HAKI YETU ameisihi serikali kuziba mianya ya ufisadi ambayo hupelekea taifa hili kupoteza takriban shilingi bilioni 700 kwa mwaka, badala ya kuongeza ushuru kwa wananchi.

Victor Kaudo mwanaharakati wa shirika la Malindi Social Justice, amemtaka rais dkt. William Ruto kutilia maanani maisha ya wananchi wa tabaka la chini, kwa kuwaondolea mapendekezo ya kuwaongezea ushuru.

Hata hivyo amewataka wabunge kuuangusha mswaada huo, ili wananchi wa tabaka la chini waweze kutoa maoni yao kuhusu mswaada huo wa fedha wa mwaka 2023.

Kwa upande wake mkereketwa wa haki za binadamu Magdalene Thuva ameelezea masikitiko yake kufuatia pendekezo la ongezeko la ushuru hatua anayodai kuwa inalenga kuwagandamiza wananchi wa kawaida.

BY ERICKSON KADZEHA