Wakiongea na wanahabari nje ya majengo ya mahakama ya Mombasa muda mfupi tu baada ya mahakama kuwaachilia huru kwa dhamana, viongozi hao wamesema na wataendelea na majukumu ya kutetea wananchi na kuikosoa serikali.
Wakati huo huo viongozi mbalimbali wamejitokeza kupongeza uamuzi wa mahakama wa kuwaachilia kwa dhamana mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga pamoja na spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire na wengine wawili.
Wakizungumza nje ya majengo ya mahakama ya Mombasa seneta wa kaunti ya Mombasa Mohamed Faki amekashifu hatua ya baadhi ya viongozi katika mrengo wa upinzani kukamwatwa na kuzuiliwa bila kuwasilishwa mahakamani kwa muda ufaao akisema ni ukiukaji wa katiba
Faki amekemea hatua ya maafisa wa usalama kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji akisisitiza kuwa waliotekeleza hayo watakabiliwa kisheria huku akiongeza kuwa wataendelea kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuandamana .
Kwa upande wao mawakili wa washtakiwa wakiongozwa na Dastan Omari wameeleza kuskitishwa kwao na jinsi idara husika ilivyowakabili viongozi hao akidai kuwa wamehangaishwa kwa muda mrefu pasi na kutilia maanani vyeo vyao.
Aidha wametaja matukio hayo kama njia ya kupoteza fedha na rasilimali za taifa akisema kuwa pesa hizo kuwa zingeelekezwa katika ujenzi wa taifa.
Itakumbukwa kuwa viongozi hao wawili na maafisa wengine wawili walikamatwa Jumatano wiki iliyopita eneo la Mtwapa kaunti ya Kilifi kwa madai ya kukusanyika na kuandamana kinyume cha sheria.
Wameachiliwa kwa dhamana ya shilling laki moja au kima cha elfu hamsini pesa taslimu kila mmoja.
BY EDITORIAL DESK