HabariNews

Mshukiwa wa Mauaji ya Afisa Mkuu wa Kaunti ya Kilifi Kusalia Korokoroni Siku 14

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Afisa Mkuu wa kaunti ya Kilifi atasalia korokoroni kwa siku 14 zaidi.

Jaji Justus Kituku amekubali ombi la upande wa mashtaka la kumzuia Diana Naliaka kwa siku kumi na nne ili kuwapa maafisa wa usalama nafasi ya kukamilisha uchunguzi wa swala hili.

“Nimesikiliza ombi la Kiongozi wa Mashtaka kutaka muda zaidi kumzuilia mshukiwa ili kukamilisha uchunguzi wao. Sina pingamizi kwa hilo nikizingatia uzito wa kesi hiyo,” akasema hakimu Kituku.

Mwendesha mashtaka Bi. Winnie Atieno alikuwa ameiomba mahakama Naliaka ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya Afisa Mkuu wa Uvuvi na Uchumi Samawati kaunti ya Kilifi, Rahab Karisa.

Rahab aliuawa kwa kudungwa kisu nyumbani mnamo Alhamisi, Julai 20, 2023.

Inadaiwa mtafaruku ulijiri baada ya Afisa huyo kurejea nchini kutoka Italia alikohudhuria mkutano muhimu wa kimataifa na akapata kiasi fulani cha pesa zake zilikuwa zimepotea nyumbani.

Naliaka aliyetoweka kufuatia kisa hicho alikamatwa Jumanne alfajiri Julai 25 huko mpaka wa Busia akijaribu kutorokea taifa jirani la Uganda.

Kesi dhidi ya mshukiwa huyo itatajwa Agosti 17 mwaka huu.

BY EDITORIAL DESK