Serikali ya kitaifa imelipa madeni yote iliyokuwa ikidaiwa na serikali za kaunti hapa nchini.
Raisi William Ruto ametangaza kuwa serikali yake imelipa mgao wa mwezi wa Julai kwa kaunti zote 47.
Akizungumza katika ibada ya Jumapili huko Ukunda kaunti ya Kwale kiongozi huyo wa taifa amesema kuwa sasa ni wakati wa magavana kutekeleza majukumu yao kwa kuwahudumia wananchi.
“Kwa mara ya kwanza tangu tuwe na katiba mpya pesa zote za kaunti tumelipa kwa wakati wake, pesa zote za CDF tumelipa kwa wakati wake.Mwezi huu tumeweka historia kwamba pesa za kaunti ya mwezi wa saba tumelipa ndani ya mwezi wa saba,” ameeleza Ruto.
Vile vile, rais ameahidi kuboresha sekta ya uchimbaji madini na uchumi samawati nchini kwa kuzindua miradi mbalimbali katika ukanda wa pwani.
Miongoni mwa mikakati ambayo serikali inapania kutekeleza ni pamoja na kuzindua viwanda vya kutayarisha na kuhifadhi samaki pamoja kutengeneza vyombo vya baharini ikiwemo boti za uvuvi miongoni mwa mingine.
“Kwa sababu ya shughuli ya maendeleo ya Pwani, kati ya mambo muhimu hapa pwani ni uchumi wa madini na uchumi samawati, ndio uti wa mgongo wa uchumi wa kaunti zetu za hapa pwani na ndio sababu tuko na mpango mzima maalum ya kuhakikisha ya kwamba sekta ya blue economy tunaipanua ili ichangie uchumi wa kenya na uchumi wa sehemu hii ya Pwani.” Ameongeza Ruto.