HabariNews

Kizaazaa Mahakamani Mhubiri tata Makenzie na wenziwe wakikariri ‘Haki Yetu’

Hali ya tafrani imeshuhudiwa katika Mahakama Kuu ya Shanzu kaunti ya Mombasa baada ya Mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na washukiwa wenza 28 kudai haki yao.

Washukiwa hao wa mauaji ya halaiki katika msitu wa Shakahola walionekana kuinua mikono juu wakirudilia kauli “ haki yetu! Haki yetu, haki yetu!”

Walianza kuzua rabsha hizo muda mfupi tu baada ya Kiongozi wa mashtaka Jami Yamina aliposimama kuzungumza, wakihisi kuwa

Mackenzie na washirika wake ambao wamefikishwa tena mahakamani hii leo, wametatiza shughuli za mahakama kwa muda wa dakika kadhaa wakidai kuhangaishwa na maafisa wa usalama kwenye seli wanakozuiliwa kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Ilibidi Wakili wa washukiwa hao Wycliff Makasembo kuingilia kati kuwatuliza, ili kupisha shughuli za kesi ziendelee. “Kwa heshima ya mahakama na kwangu mimi kama wakili wenu, ninawasihi mtulie Mahakama itasikiliza malalamishi yenu.  Mahakama imewasikia, tafadhali kaeni chini,” akawaambia Bw.  Makasembo.

Aidha, wamedai kulazimishwa kulala sakafuni huku baadhi wakidai kuvalia sare za wafungwa hata kabla ya kuhukumiwa.

Ikumbukwe kuwa mwezi uliopita mahakama hiyo ya Shanzu ilimwachilia mkewe Mackenzie, Bi. Rhoda Maweu Mumbua kwa dhamana ya shillingi 400,000.

Mackenzie na wenziwe  watasalia kizuizini kwa siku 3 zaidi baada ya Hakimu Mkuu wa Mahakama hiyo Yusuf Shikanda kuamua hivyo, muda ambao watarejea kujua hatma yao iwapo watafunguliwa mashtaka au la.

Awali upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina ulikuwa umeomba mahakama muda wa siku 47.

Upande wa mashtaka hata hivyo umekubaliana na muda huo wa siku 3 uliotolewa na mahakama kumalizia majadiliano zaidi.

BY EDITORIAL DESK