Mrengo wa Serikali, Kenya Kwanza umewateua wawakilishi watano watakaowawakilisha katika mazungumzo ya maridhiano yanayotarajiwa kufanyika baina yao na mrengo wa upinzani.
Katika taarifa yake Kenya Kwanza imetangaza kuwa watano hao wataongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, Kiongozi mwenza katika Bunge la Seneti Aron Cheruiyot na gavana wa Embu Cecily Mbarire.
Wengine katika kikosi hicho ni mbunge wa Bungoma Catherine Wambilianga na naibu mwenyekiti wa chama cha UDA Hassan Omar Sarai ambaye pia Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki wakikamilisha jopo hilo.
Aidha Kenya Kwanza imetangaza ajenda zao watakazojadili na Upande wa Upinzani na kusisitiza kuwa hakutakuwa na majadiliano yoyote yanayohusiana na ushirikiano na ugawaji mamlaka maarufu kama ‘hand shake’.
Haya yanajiri siku chache baada ya muungano wa Azimio kutangaza wawakilishi wake katika mazungumzo hayo ya maridhiano huku wakisema kuwa hawataruhusu chama chochote kuamua kuhusu ajenda zitakazojadiliwa.
Upande wa mrengo wa Azimio awali uliteuwa wawakilishi wao watano watkaongozwa na Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
BY EDITORIAL DESK.