Mhubiri tata Paul Makenzie sasa anadai kuteswa katika gereza la Shimo la Tewa ambako amekuwa akizuiliwa na washukiwa wenzake 17.
Kupitia wakili wake Wycliffe Makasembo, Makenzie aliyefikishwa mahakamani Ijumaa Agosti 4 na washukiwa wenziwe aliibua madai kuwa huenda chakula ambacho amekuwa akipewa katika gereza hilo kimekuwa kikiwekwa sumu.
Kulingana na Mackenzie, ametengwa na wenzake na kuwekwa kizuizini peke yake hali ambayo inamtia hofu kwamba huenda kuna njama fiche dhidhi yake.
Mhubiri huyo aidha alisema kuwa kila mara maafisa wa gereza hilo wamekuwa wakizuru seli anakozuiliwa wakiwa na vitoza machozi asijue kiini cha nia yao.
Mackenzie aliitaka Mahakama hiyo imhamishie hadi kituo cha Polisi cha Mtwapa au kingine katika kaunti ya Kilifi iwapo ataendelea kuzuiliwa.
Haya yalibainika kwenye kikao cha kubaini iwapo Mackenzie na washukiwa wenza 17 wataendelea kuzuiliwa kwa siku 47 zaidi au la.
Huku hayo yakijiri Mahakama ya Shanzu Ijumaa Agosti 4, iliwafutia mashtaka ya kutaka kujiua washukiwa 65 wa kikundi cha manusura wa Shakahola ambao walikamatwa kwa kujaribu kujinyima kula hadi kufa.
65 hao waliokolewa kutoka msitu wa Shakahola na kupelekwa kituo cha uokoaji ambako kwa siku kadhaa pia walikataa kula.
Upande wa Mashtaka katika kesi hiyo umesema washukiwa hao sasa watakabiliwa na mashtaka ya mauaji na ukatili kwa watoto wao kujiunga na dhehebu hilo tata ililopelekea vifo vya baadhi ya watoto.
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Jami Yamina ameieleza Mahakama hiyo kutokana uchunguzi unaoendelea washukiwa hao walistahili kushtakiwa kwa makosa hayo.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Shanzu Joe Omido ameagiza washukiwa hao kurudishwa mahakamani Alhamisi, Agosti 10 mwaka huu.