Mazungumzo baina ya vyama vya walimu nchini KNUT na KUPPET pamoja na mwajiri wao Tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuhusu nyongeza za mishahara ya walimu yaligonga mwamba Jumanne Agosti 22, 2023.
Hii ni baada ya vyama vyote viwili kuhitaji vipewe muda zaidi kutathmini kwa kina mapendekezo yote ya tangazo lililotolewa na tume ya kutathmini mishahara ya wafanyakazi wa umma SRC kuhusu nyongeza ya mishahara ya walimu kati ya asilimia 7 hadi 10.
Vyama hivyo vinavyoongozwa na makatibu wakuu Collins Oyuu na Okello Misori, vilibaini kwamba vitahitaji muda zaidi kuyaangazia mapendekezo yaliyomo kwenye mazungumzo hayo na mawakili wao kabla ya kuamua iwapo watatia sahihi au kukataa mapendekezo hayo.
“Tulipata taarifa kuwa SRC haikuwa tayari kuwajibikia nyongeza iliyokuwepo ya kati ya aslimia 7 na 10, KNUT isingeweza kuafiki makubaliano hayo tulisimama kidete na tumesema hatutakubali chochote kutoka kwa SRC kinyume cha makubaliano yetu.” Alisema Katibu Oyoo wa KNUT.
KNUT na KUPPET vimekuwa vikishinikiza nyongeza ya mishahara ya walimu hadi asimia 70 ili kuwiana na kuongezeka kwa gharama ya maisha nchini.