Miaka 60 baada ya Kenya kupata uhuru wakazi wa vijiji vya Mkuyuni na Mwambao huko kaunti ya Kwale wangali gizani wakisubiri kufikishiwa nguvu za umeme.
Wakazi hao walilalamikia kutelekezwa na viongozi pamoja na serikali kwa muda mrefu huku wakitishia kuandamana hadi ofisi ya mbunge wa Lunga Lunga ili kushinikiza kuwekewa nguvu za umeme vijijini mwao.
Kulingana na wakaazi hao, kiza hicho cha muda mrefu kimechangia pakubwa kuzorotesha Maendeleo na ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo. Waliongea haya wakati wa kuzindua rasmi jopo litakalofatilia hatua ya upatikanaji wa nishati hio inayowarudhisha nyuma kwa sasa.
“ katika vijiji hivi vyetu viwili vilitengwa kabsaa kuhusu mambo ya stima, wenzetu stima ilipita ikaenda shimoni lakini kwetu tumerukwa kabisaa” alilalama mkaazi
“kama mimi kwamba nimetegemea bahari mvuvi aje na samaki nipate niweke kwa friji nifanye biashara, lakini ukiangalia sasa itabidi ununue madonge ya barafu uweke na hizo ni pesa ambapo wavuvi wakikosa samaki barafu inakuwa wasted lakini kama kungekuwa na stima ningezima tu friji yangu nikawekeza malipo Zaidi.” Alisema mwingine.
Abubakari Asriin na Hamisi Abdallah walibaini kuwa ukosefu wa umeme umewapelekea wana wao kuathirika kielimu. Hili limepelekea wengi kuchukua mikopo ya sola jambo wanalotaja kuwa ghali mno
“Leo ikiwa umeshindwa na shilingi hamsini ya kulipia solar inabidi sasa moto hakuna hata motto kustadi hawezi stadi, miskiti haina stima tukisema tufanye printing ya makaratasi ya masomo ya watoto inakuwa ni kazi, twalipa pesa nyingi ukimaliza kulipa kifaa nacho kimeisha nguvu” Walilalama .
Wakaazi hao sasa wanamuomba Rais William Ruto na wahisani kuingilia kati kutegua kitendawili hicho ili kuwatoa kwenye giza lililodumu na kuwahangaisha kwa muda mrefu.
BY EDITORIAL DESK